Samia kufungua uchumi ukanda wa kusini

Ruvuma.  Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendeleza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania, akisisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana chini ya ilani ya mwaka 2020/2025 yamejenga msingi imara kwa ahadi mpya zinazolenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi katika eneo hilo.

Akizungumza leo Jumapili Septemba 21, 2025 mbele ya maelfu ya wananchi wa Mbamba Bay wakati wa mkutano wa kampeni amesema Nyasa itapa miradi mikubwa mitatu ya kimkakati itakayoifungua wilaya hiyo kiuchumi na kuiunganisha na nchi jirani.

 “Septemba mwaka jana nilifika hapa ikiwa ni sehemu ya ziara, nilikagua na kuzindua miradi mbalimbali kama utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025. Tumefanikisha mengi, ndiyo maana tunarudi tena tukiwa na ujasiri wa kuinadi ilani mpya,” amesema.

Miongoni mwa miradi aliyoitaja ni ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay ulioanza baada ya yeye kuweka jiwe la msingi  Septemba mwaka jana.

Pia, amebainisha utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri na kwamba ndoto ya muda mrefu ya wakazi wa Nyasa ya kuwa na bandari ya kisasa,iko mbioni kutimia mapema mwaka ujao.

Mradi mwingine ni wa Barabara ya Mbinga–Mbamba Bay yenye urefu wa kilomita 66, inatumika kama kiunganishi muhimu kati ya Bandari ya Mtwara na Mbamba Bay na kusaidia kuimarisha usafirishaji wa bidhaa na abiria.

Vilevile, mgombea huyo ametaja kukamilika kwa Bandari ya Ndumbi, ambayo kwa sasa inahudumia shehena ya hadi tani 110,000 kwa mwaka, kutoka tani 40,000 za awali.

Mbali na mizigo amesema idadi ya abiria wanaohudumiwa nayo imeongezeka kutoka 45,000 hadi kufikia 100,000 kwa mwaka.

“Haya ni maendeleo makubwa. Bandari hii ni ya kimkakati kwa kuwa inarahisisha usafiri wa watu na bidhaa, na kuchochea biashara katika eneo hili,” amesema.

Katika kuendeleza maono ya maendeleo ya ukanda wa kusini, mgombea huyo alitangaza pia mpango mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa ya kilomita 1,000 kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay.

Amesema reli hiyo ni sehemu muhimu ya mkakati wa maendeleo ya kusini na uchumi wa viwanda wa Tanzania, ikilenga kuongeza biashara, kufungua fursa za uwekezaji kwenye migodi na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na Msumbiji, Zambia na Malawi.

Pia, amesema reli hiyo itapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya nafaka na kuunganisha maeneo ya kiuchumi ya Liganga na Mchuchuma, maarufu kwa rasilimali za chuma na makaa ya mawe.

“Tayari tumekamilisha tafiti za awali na tupo katika hatua za makubaliano ya kuanza ujenzi. Tukifanikiwa, reli hii italeta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa ukanda huu,” amesema Samia.

Kuhusu ajira amesema chama chake kimekusudia kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao kwenye wilaya zote hatua itakayotengeneza ajira kwa vijana.

“Kwa hapa Nyasa tunakwenda kufunga mtambo wa kukaushia samaki, pia tutafunga mtambo wa kukoboa kahawa ili kuongeza thamani. Niwaombe sana wabunge na madiwani wayasimamie haya ili yawafae wananchi hususani kutengeneza ajira kwa vijana.

“Kwa namna Nyasa inavyokuwa tunafikiria iwe na soko kubwa, soko hili litakuza mapato na kuwaongezea fursa wananyasa sambamba na kuwahudumia raia wa nchi jirani za Malawi na Msumbiji na wale wanaovuna dagaa wataweza kupata wateja wengi na bei nzuri,” amesema.

Kwenye sekta ya uvuvi amesema Serikali  itaendelea kutoa vifaa vya kisasa ikiwamo boti maalumu ya wokozi katika Ziwa Nyasa.

Kutokana na ahadi hizo, Samia amewataka wananchi wa Nyasa kuendelea kuiamini CCM, akiahidi kuwa Serikali ya chama hicho itaendelea kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kasi, tija na weledi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, mgombea mwenza wa urais kupitia tiketi ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema anamshukuru Samia kwa imani aliyomuonesha kwa kumteua kuwa mgombea mwenza akimuahidi atakuwa msaidizi mwaminifu.

“Huu ndio mkoa wangu wa nyumbani na kwa mara ya kwanza nazungumza nao katika mkutano huu wa kampeni, nakushukuru kwa heshima na imani kubwa uliyonipa ya kunipendekeza kuwa mgombea mwenza. Hii si heshima yangu peke yangu bali mkoa wa Ruvuma.

“Kwa mila zetu Mkoa wa Ruvuma imani huzaa imani, nitakusaidia kwa imani yangu na uwezo wangu wote, kuhakikisha unatekeleza imani ya CCM kama ulivyokusudia ,” amesema.

Akiwa wilayani Mbinga Samia ameahidi endapo atapata ridhaa ya kuongoza miaka mingine mitano Serikali itafanya jitihada za kuimarisha masoko ya mazao na kuendelea kutafuta bei bora ili mkulima afaidike na nguvu zake.

Samia ametoa ahadi hiyo wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika leo, Septemba 21, 2025 wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.

Amesema anatambua wilaya hiyo inafanya vizuri katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara, hivyo Serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa kuhakikisha wakulima wananufaika na jasho lao.

“Nafahamu Mbinga ni kituo kizuri na muhimu kwa uzalishaji wa mazao, tunataka kuhakikisha shughuli hii kubwa mnayofanya mnanufaika nayo, ahadi yangu kwenu ni kuhakikisha tunaimarisha masoko na kupata bei bora.

“Kingine tuendelee kutoa ruzuku ya pembejeo na mbolea na muhimu zaidi tutatoa huduma za ugaini, tutakuwa na BBT ya ugani tutawatumia vijana walio na taaluma ya ugani kutoa huduma hizo, lengo hapa ni kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri zaidi upande huo,”amesema.

Kwa upande wa miundombinu, Samia amesema Serikali itaendeleza ujenzi wa barabara kadhaa za wilaya hiyo katika viwango mbalimbali vitakavyoruhusu kupitika kwa mwaka mzima.

Pia, ameahidi kujenga Daraja la Mto Lumeme na kuunganisha na barabara zake.

“Niwaambie ndugu zangu hakuna mradi ghali kama barabara, kilomita moja gharama yake ni vituo viwili vya afya na ndiyo maana hatuendi kwa kasi sana. Ahadi yetu ni kuwatumikia na mkitupa ridhaa ya kufanya kazi, tutakwenda kuinua utu wa Mtanzania, utu wa kila mmoja bila kujali dini wala kabila lake,”amesema mgombea huyo.

Katibu Mkuu wa CCM Dk Asha-Rose Migiro amesema wananchi wameridhishwa na maendeleo yanayotokana na utekelezaji wa ilani ya mwaka 2020/2025.

“Kuyaendeleza hayo mazuri tunaomba mumpe tena mgombea wa CCM ridhaa ya miaka mitano ili akaendeleze kazi ya kutuletea maendeleo kwenye Taifa letu,” amesema Dk Migiro.

Mgombea ubunge wa Mbinga Vijijini, Judith Kapinga amesema watu wa jimbo hilo walikuwa wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 50 kufuata huduma za afya lakini sasa kuna hospitali ya wilaya na vituo vipya vya afya vimejengwa pamoja na zahanati 17.

Akizungumzia pia namna kahawa ilivyokuza uchumi wa wakazi wa Mbinga Vijijini, Judith amesema miaka mitano iliyopita kilo moja ya kahawa iliuzwa Sh3,600 lakini sasa bei imefikia Sh11,800 hadi Sh12,100.

“Sisi watu wa Mbiga Vijijini hatukuzoea kuyaona haya maendeleo yamekuwa kwa kasi sana, tumejengewa shule za msingi na sekondari pamoja na mabweni na nyumba za walimu. Kwa mambo haya mazuri hatuna cha kufanya zaidi ya kutiki itakapofika Oktoba 29.

“Ukija kwenye eneo la umeme zaidi ya vitongoji 300 vya Mbinga Vijijini vina nishati ya umeme, hatuna mashaka, upande wa barabara Tarura peke yake kwa kipindi cha miaka minne tumepewa bilioni 15,” amesema Judith.

Mgombea ubunge wa Mbinga Mjini, Jonas Mbunda amesema wananchi wa jimbo hilo  wameguswa na upatikanaji wa maji ikiwa ni matokeo ya kuboresha miundombinu ya maji iliyogharimu Sh14 bilioni.

“Hatuna cha kusema katika eneo hili la maji, hata hivi karibuni kulipokuwa na upungufu tumepewa tena Sh4.6 bilioni ambazo zimetumika kuongeza vyanzo vya maji. Vijiji vyote 78 vya Mbinga Mjini vina umeme, upatikanaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa kahawa umeongezeka hatuna cha kukulipa zaidi ya kuhakikisha unapata ushindi wa kishindo,”amesema.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Odo Mwisho  amesema amejipanga kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo akiahidi mkoa huo utaongoza kwa kupata kura nyingi za mgombea wa urais.

Mratibu wa kanda ya kusini na mjumbe wa kamati kuu, Laila Ngozi amesema wananchi wana imani kubwa na wagombea wa CCM kwa kuwa watasimamia kikamilifu ilani ya mwaka 2025/2030.