Serikali itaendelea kuboresha mitalaa sekta ya elimu- Mahundi

Rungwe.  Naibu Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali itaendelea kuboresha mitalaa ya elimu nchini ili kuwezesha vijana kujiajiri, hasa watoto wa kike.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumapili Septemba 21, 2025, alipokuwa akizungumza katika mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya Wasichana ya Joy, Kata ya Ndato, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya.

“Nimefurahishwa kuona kiwango kikubwa cha taaluma kwa wahitimu, pamoja na ukuaji wa teknolojia bunifu zitakazowasaidia kujiajiri wanaporudi kwenye jamii,” amesema Mahundi. Pia, amesema uwekezaji mkubwa wa Wizara ya Elimu unalenga kuhakikisha vipaji vya vijana vinatimizwa na kuzaa wataalamu katika fani mbalimbali.

Pia, amewataka wazazi kuwa chachu ya kudhibiti matumizi holela ya mitandao ya kijamii wakati huu ambao Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Mkurugenzi wa shule hiyo, Tito Tweve amesema  mbali na mahafali hayo, shule hiyo imepokea mtalaa mpya wa elimu na kuanza kuandaa vijana katika stadi za maisha.

Wakizungumza na Mwananchi kwenye sherehe hiyo, baadhi ya wanafunzi akiwamo, Annastella Kipeta ameelezea umuhimu wa masomo ya sayansi.

Amesema masomo ya sayansi ni fursa kubwa ya kukabiliana na soko la ajira kupitia bunifu mbalimbali, kama uzalishaji wa nishati ya hewa ya oksijeni, ujenzi wa miundombinu na bandari za kisasa.

Mwanafunzi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Prisca Bruno amesisitiza haja ya Serikali kuunda mazingira wezeshi kwa shule za sekondari zenye mitalaa ya sayansi ili kuzalisha wataalamu wenye uwezo watakaosaidia kumaliza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.

Bress Safari, mwanafunzi wa kidato cha tatu amewatahadharisha wenzake kuacha kuiga wengine mitandaoni badala yake, watimize ndoto zao za elimu ili kuwa tegemeo kwa Taifa.