Canada. Visa vya matajiri wakubwa watatu duniani na marais wawili wa Marekani vinasisimua, kufikirisha, na vinafundisha kwa wenye akili na busara.
Marehemu Steve Jobs, mwanzilishi wa kampuni kubwa ya Apple, Jeff Bizos wa Amazon, na Larry Elison wa Oracle wanaweza kutufundisha kitu juu ya nani anapaswa au anaadhibiwa kati ya wazazi na watoto waliozaliwa nje ya ndoa.
Hawa wote watatu wana sifa zinazofanana. Mosi, wote ni wanaume. Pili, ni wazungu. Tatu, ni wamarekani. Nne, wote walitelekezwa na baba zao. Na tano, wote ni mabilionea.
Sita, wote wamethibitisha kuwa jiwe kuu la pembeni lililokataliwa na waashi, maana, baba zao waliowatelekeza walikuja kujigonga kwao baada ya kufanikiwa.
Ni wangapi unaowajua kama hawa hata kama siyo mabilionea? Mfano, mwingine ni wa marais wawili wa Marekani Bill Clinton na Barack Obama waliotelekezwa na baba zao wakatokea kuwa watu mashuhuri sana duniani.
Wakati mkifikiria kuwakubali au kuwatelekeza watoto wa nje ya ndoa, jiulize yafuatayo: mjue. Si makosa yao bali yenu. Kama ni makosa, basi ni yenu. Sasa wanaadhibiwa kwa lipi?
Hivi, huwa wazazi kama hawa wanajisikiaje? Je, huwa wanajiuliza wangekuwa ni wao wangetaka watenzwe vipi? Mkuki kwa nguruwe na udhaniaye ndiye, kumbe siye. Tia maanani.
Wengi, ambao ni wanaume, huwakataa na kuwatelekeza watoto wao kwa kuogopa kuvunja ndoa zao. Unapomtelekeza mtoto, unaharibu maisha yake.
Ila matokeo, yanaonyesha kuwa unaharibu hata maisha yako mwenyewe kutokana na ubinafsi usio na kichwa wala miguu.
Kinachosikitisha, watoto hao hao wanapofanikiwa, wahusika hawa hawa waliowatelekeza huwa hawaogopi kuvunja ndoa zao. Na badala yake, hujifanya hamnazo kiasi cha kutaka misaada au heshima kutoka kwa watu waliowaumiza maishani. Huu ni nini kama siyo unyonyaji na unyama?
Kimsingi, kutokana na uzoefu na visa hivyo hapo juu, unaweza kukataa almasi ukidhani ni jiwe, na baadaye ukajikuta ukijutia kufanya hivyo hasa ikizingatiwa kuwa watoto ni malaika na Mungu hamtupi mja wake. Kwa wale waliotelekezwa, ni vizuri kuwasamehe hawa wazazi waliowatelekeza.
Ila msiwape huduma yoyote kwa vile nao waliwanyima haki na huduma. Ni wezi wa kawaida wanaoshabikia na kuvuna wasipopanda na kupanda wasipovuna. Jifunzeni.
Tuseme wazi. Hatuhimizi watu wazae nje ya ndoa au kuzaa bila mpangilio. Je, ikishatokea tufanye nini? Hili ndilo swali na somo la leo kwa wanandoa na hata wazazi wote.
Kama umemtelekeza mwanao, hata akifanikiwa, endelea kumtelekeza na si kumlaumu au kumsumbua na kumtuhumu kuwa hakujali wakati hukumjali. Kimsingi, hapa, unavuna ulichopanda. Ukipanda shubiri, usitegemee kurina asali.
Ulimfanyia dhuluma, ukatili, na unyama. Akishafanikiwa, unataka kumnyonya na kumsumbua bure. Kama ambavyo hakukusumbua, usimsumbue. Kama ulivyomsahau, asikukumbuke. Na kama ulivyomkana, si kosa akikukana. Kama ambavyo hukumjali, si vibaya asipokujali. Mechi au ngoma droo.
Japo mila nyingi za Kiafrika hata dini zinafundisha kusamehe, nani awezaye kumsamehe nyoka aliyemng’ata ili amng’ate mara ya pili na kumuachia sumu iletayo kifo?
Nani awezaye kutukuza upanga uliomkata akanusurika kimiujiza? Waingereza wana msemo usemao fool me once, shame on you. Fool me twice, shame on me, yaani, ni upumbavu kung’atwa na nyoka kwenye shimo moja mara mbili.
Wapo wengi waliolala njaa, kubagazwa na kubaguliwa kwa sababu ya kutelekezwa. Pia, wapo waliokosa fursa kama vile afya, malezi, elimu, na mengine mengi kama hayo.
Hata hivyo, kutokana na kudura za Mwenyezi Mungu walijitahidi hadi wakafanikiwa. Japo tunaweza kuwachukulia kirahisi hasa pale wanapokataa kuwasamehe waliowatelekeza.
Tujue wana mengi tusiyojua kwa sababu si rahisi kuvaa viatu vyao na kuhisi wanavyohisi hasa hasara walizopata maishani kutokana na kutelekezwa.
Je, hao hapo juu wanatufundisha nini? Hili ni funzo kwa wote waliotekelekezwa. Badala ya kupoteza muda kulaumu waliowatelekeza, waathirika, wachukie na kugeuza hasara hii kuwa faida katika maisha yao. Mfano, Jobs, aliyekutana na baba yake mzazi kwa bahati mbaya alipoulizwa kuhusiana na baba yake alisema: “Nilijifunza mambo kidogo juu yake na sikupenda nilichojifunza.” Nani anayetaka mwanae asimjue au kutofurahishwa na kutomjua?
Tumalize. Hadi anafariki dunia, Jobs, hakuwahi kupoteza muda kukutana na baba yake ambaye bado yu hai na anasema alichobaki nacho ni huzuni usio kifani kwa makosa yake.