Dar es Salaam. Wakati idadi ya mitaji na miradi inayosajiliwa nchini ikiongezeka kila siku, wawekezaji wametafutiwa namna ya kupata huduma za kifedha ili kurahisisha utekelezaji wa miradi hiyo.
Hiyo ni baada ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) kuweka saini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Benki ya Biashara Tanzania (TCB), yanayolenga kuwasaidia wawekezaji kupata usaidizi wa haraka wanapohitaji huduma za kifedha kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.
Kupitia ushirikiano huu, TCB itatoa huduma za kifedha, ikiwamo mitaji ya uendeshaji kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Hili linafanyika wakati ambao Tanzania imejiwekea lengo la kusajili miradi 1,500 ya uwekezaji mwaka 2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 60 ikilinganishwa na ile ya mwaka 2024.
Lengo hilo liliwekwa wakati ambao tayari miradi 372 ilikuwa imesajiliwa kati ya Januari hadi Mei 2025 huku sekta ya viwanda ikiendelea kuwa kinara kwa kupokea mtaji mkubwa uliowekezwa katika usindikaji wa vyakula, viwanda vya bidhaa zinazotumika sana kama sabuni, vinywaji, chuma, karatasi za vifungashio na plastiki vikipata uwekezaji mkubwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mkuu wa Tiseza, Gilead Teri ushirikiano kati yao na TCB utakwenda kuimarisha nafasi ya Tiseza kama kituo cha huduma za pamoja kwa mwekezaji.
“Lengo kuu ni kuhakikisha wawekezaji wanaweza kusajili miradi yao kwa urahisi na kupata huduma za kifedha kupitia Kituo cha Huduma kwa Mwekezaji,” amesema Teri.

Amesema mtandao wa matawi zaidi ya 80 ya TCB yanawapa uhakika kuwa wawekezaji watahudumiwa kwa haraka na ufanisi.
Kupitia mtandao huo wa matawi, sasa TCB inashika nafasi ya tatu miongoni mwa benki zinazofanya vizuri nchini.
Teri amesema TCB pia itawaunga mkono Watanzania waishio ughaibuni wanaotaka kuwekeza nyumbani, jambo litakalowawezesha kuleta mitaji nchini huku Tiseza ikihamasisha fursa za kiuchumi katika sekta za kipaumbele kama vile viwanda.
Aidha, alibainisha vivutio vilivyopo kwa wawekezaji wa ndani, vikiwamo ardhi ya bure kwa miradi ya viwanda, msamaha wa forodha kwa mitaji ya miradi hadi asilimia 100 na punguzo la ushuru wa forodha hadi asilimia 75.
Amesisitiza kuwa makubaliano hayo pia yanatoa muongozo wa taasisi hizo mbili kubadilishana ujuzi na uzoefu wa kiufundi ili kuboresha utoaji wa huduma.
Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Mihayo amesema ushirikiano huo unaendana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeyataka mashirika ya umma kushirikiana ili kuongeza tija na kuzalisha mapato yasiyo ya kodi.
“Hadi sasa benki yetu ina matawi 82 na tumejipanga kuongeza matawi 10 zaidi kila mwaka,” amesema.
Ongezeko la matawi linaenda sambamba na ukuaji wa benki kidigitali, hadi sasa TCB ina mawakala 7,000 na inapanga kuongeza mawakala wengine 3,000 mwaka huu.