Wanawake wanapovunja ukimya wa hisia, wanawake nao wanaweza kuwatokea wanaume

Katika jamii nyingi za Kiafrika, kumekuwa na mtazamo wa muda mrefu kwamba jukumu la kumtongoza mpenzi ni la mwanaume pekee. Hata hivyo, hali kiuhalisia, wanawake nao wanaweza kuwa mwanzo wa kusababisha  uhusiano. 

Wanawake wanazidi kuthibitisha kuwa nao wana haki na uwezo wa kuonyesha mapenzi kwa mtu wanaowapenda, bila kuona haya au kuhisi wanavunja mila.

Diana Mugowe, mshauri wa uhusiano anasema kuwa wanawake wengi wamekuwa wakinyimwa fursa ya kuwa wazi na hisia zao kwa sababu ya hofu ya kuhukumiwa.

 “Jamii imewafundisha wanawake kuwa wakisubiri kutongozwa ndio wanaheshimika. Lakini kizazi kipya kinaanza kuvunja mipaka hiyo,” anasema.

Mkazi huyu wa jijini Dar es Salaam na baba wa watoto watatu, ana ushuhuda  wa namna wanawake wanavyoweza kuanzisha uhusiano, tofauti na wengi wanavyofikiri. Anasimulia:

“Unaposikia mwanamke anaweza kumtokea mwanamume usione jambo la ajabu. Mimi maishani mwangu naweza kusema nina a kind of good luck (Nina bahati). Wanawake wawili walishawahi kuni face ( kunikabili) uso kwa uso wakitaka niwe na uhusiano nao ili niwaoe. 

“Yaani mimi mwanamume mzima nabananishwa katika mazungumzo nabembelezwa, naombwa nikubali. Ilikuwa mtihani sana na nilishangaa maana mmoja alikuwa mdogo sana kwangu kiumri, nikajiuliza kapata wapi nguvu ile ya kunitongoza, yaani aliniweka kati akinibembeleza kama saa moja hivi.  Huyu wa pili nilimkatalia akaanza kulia nikamuonea imani ikabidi nikubali hivyohivyo tu. Dah! Sitosahau matukio haya.”

Katika mazungumzo na gazeti hili, baadhi ya wanawake walieleza kuwa wamewahi kuwafungukia wanaume wanaowapenda na hawakujutia uamuzi huo. Joyce Mwaikenda, mfanyabiashara jijini Mbeya, anakiri kuwa alimtongoza mume wake miaka sita iliyopita.

“Nilimueleza wazi jinsi nilivyompenda. Kwa bahati nzuri, naye alikuwa ananihisi hivyo ila alikuwa na wasiwasi kuniambia. Leo hii tuna ndoa yenye furaha,” anasema.

Mitandao ya kijamii pia imechangia kwa kiasi kikubwa kubadilika kwa mtazamo huu. 

Katika majukwaa kama Instagram, X (zamani Twitter), na TikTok, wanawake wanatumia nafasi hizo kumweleza mtu wanayempenda hisia zao kwa njia ya ubunifu kama vile video, picha au hata ujumbe wa moja kwa moja (DM). 

Aidha, wataalamu wa saikolojia wanaeleza kuwa kutongoza si suala la kijinsia bali ni mawasiliano ya kihisia kati ya watu wawili. Dk Jane Mbonela, mtaalamu wa saikolojia, anasema kuwa kutongoza ni kuonyesha nia ya kuwa na uhusiano wa karibu na mtu mwingine. 

“Ikiwa mwanamke anahisi kuwa amevutiwa, ana haki ya kueleza hisia zake. Hii ni sehemu ya usawa wa kijinsia tunaoendelea kuupigania,” anasisitiza.

Lakini je, wanaume wanalipokeaje suala hili? Joseph Mutua, mkufunzi wa mafunzo ya uhusiano, anaeleza kuwa wengi wao wanapokea vizuri kutongozwa na wanawake. 

“Wanaume pia huwa na hofu ya kukataliwa, hivyo inapotokea mwanamke anaanza mazungumzo au kuonyesha nia, huleta urahisi wa kuanzisha uhusiano,” anasema.

Pamoja na hayo, bado kuna changamoto zinazowakumba wanawake wanaotongoza. 

Baadhi ya wanaume huwadhania wanawake hao kuwa ‘wasio na maadili’ au ‘wanaojitupa’. Hili linaonyesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuelimisha jamii kuhusu usawa wa kijinsia na kubadili mitazamo potofu.

Hali hiyo pia inaonekana katika maeneo ya kazi, vyuo vikuu na hata katika hafla za kijamii. Mwanamke anapomwambia mwanaume kwamba anampenda, mara nyingi hushangazwa au hata kubezwa. Hii ndiyo sababu baadhi ya wanawake bado wanajizuia hata kama wanahisi kupenda.

Hata hivyo, wanawake waliothubutu kutongoza wanasema kuwa hatua hiyo imewawezesha kuwa na uhusiano wa kweli na wenye mawasiliano ya wazi. Wengine hata wanashauri wanawake wenzao kuacha kusubiri na kuchukua hatua kama wanahisi ni sahihi kufanya hivyo.

Katika ulimwengu unaobadilika kila siku, ni wazi kuwa dhana ya nani anatakiwa kuanzisha uhusiano inapaswa kupitiwa upya. Mapenzi si suala la jinsia moja. Wanawake, kama wanaume, wana hisia, wanapenda, na wanastahili nafasi ya kusema kile wanachohisi bila kuogopa hukumu.

Kadiri jamii inavyoendelea kukumbatia usawa wa kijinsia, ni wazi kuwa wanawake watakuwa huru zaidi katika kuonyesha mapenzi yao. Kutongoza si kudhalilisha, bali ni ujasiri wa kueleza hisia. Ni wakati wa kuvunja miiko na kuruhusu kila mtu awe huru kumpenda anayempenda.