Mbeya. Wakati joto la uchaguzi mkuu likizidi kupanda nchini, Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo nchini (Chawata) Mkoa wa Mbeya kimesema amani na usalama unahitajika kuliko kitu kingine kwani hali ikichafuka wao ndio waathirika wa kwanza.
Pia, kimeomba vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi kutoa fursa kwa watu wenye ulemavu wa viungo ili kupata wawakilishi watakaoweza kuwasilisha kero na changamoto zinazowakabili.
Akizungumza leo Septemba 21, 2025 katika uzinduzi wa makala maalumu, mwenyekiti wa chama hicho, Evance Mwakyusa amesema vyama vinavyoshiriki katika uchaguzi mkuu vinapaswa kutoa fursa kwa watu wenye ulemavu.
Amesema kinachowapa matumaini ni namna kundi hilo lilivyopata wagombea kwa baadhi ya vyama, hivyo kwa sasa wanaomba amani ili uchaguzi uishe salama.
“Amani ikipotea sisi ndio tutaumia kwa kuwa hatuna mbinu zozote za kujipambania, tuviombe vyama vyote kutoa fursa kwa kundi letu ili tupate wa kutusemea.”
“Lakini pamoja na sisi kuwa walemavu, hata wengine ni walemavu watarajiwa, hali ikishakuwa mbaya haiangalii nani mzima, kimsingi kila mtu atambue amani ndio msingi wa maendeleo,” amesema Mwakyusa.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo ameongeza kuwa kumekuwapo na changamoto ya watu wenye ulemavu wa viungo kutochangamkia mikopo ya asilimia 10 kutokana na kukosa elimu juu ya fedha hizo.
Amesema kauli ya Serikali juu ya kutoa mkopo kwa mtu mmoja mmoja, inatoa matumaini mapya kwa kundi hilo, akiwaomba wenye hali hiyo kuchangamkia nafasi hiyo ili kujikwamua kiuchumi badala ya kubweteka.
“Elimu itolewe badala ya kufikiri kwamba mlemavu ni wa kusaidiwa muda wote, wanahisi mikopo ni sadaka au mgawo, nitoe rai kwa wenzangu kujitokeza kuomba mikopo hiyo ili wajikimu kimaisha,” amesema mwenyekiti huyo.
Jumanne Mwakilasa amesema kinachowapa ugumu wa kuchukua mikopo ni kutokana na dhana iliyojengeka tangu zamani ya walemavu kutopewa elimu ya utambuzi na kujenga hofu na woga kuomba mkopo.
Amesema kutokana na hali hiyo, baadhi ya watendaji kuwadharau walemavu na kushindwa kuwasaidia namna ya kukabiliana na maisha yao ya kila siku, akiomba elimu ifike ngazi za chini hususan vijijini badala ya kuishia mjini.
“Walemavu wameishi bila elimu, wengine walifichwa ndani hali iliyowaweka katika mazingira magumu na kushindwa kujitegemea, zaidi iliwafanya baadhi ya viongozi kutowathamini na kuwaheshimu badala yake wanabezwa, tupewe elimu ya mikopo tuweze kufanya kazi,” amesema Mwakilasa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, Ofisa Tawala wa wilaya hiyo, Devotha Chacha amesema Serikali imewapa nafasi sana makundi ya walemavu katika nyanja ya uongozi na mikopo.
Amesema kutokana na umuhimu wa kundi hilo, Serikali imetoa kipaumbele kwa kundi hilo kuomba mkopo kwa mtu mmojammoja badala ya kutumia kundi akiwaomba kuchangamkia fursa hiyo.
“Zipo fursa nyingi mnazoweza kuzitumia ikiwamo ubunifu na uthubutu wa kuendesha maisha badala ya kujikatia tamaa kwamba ni mlemavu, Serikali imefungua milango mingi kwa ajili yenu, msijifungie nyumbani na Oktoba 29 jitokezeni kupiga kura,” amesema Devotha.