Yanga yarudi na siri kutoka Angola

WAKATI kikosi cha Yanga alfajiri ya leo Jumapili kikiingia Dar es Salaam kikitoka Angola, kuna kitu ambacho kocha wa timu hiyo, Romain Folz anatamba nacho huku mwenyewe anasema bado yupo katika kuijenga timu imara msimu huu.

Wakati Folz akiyasema hayo, kuna siri imefichuka huku Yanga ikiwa tayari imefanya mambo makubwa katika mechi mbili za kimashindano, moja ikiwa ni Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba.

Katika mechi hizo mbili ambazo ni Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Wiliete Benguela, Yanga imeshinda zote huku ikibadili kikosi cha kwanza.

Ukiangalia vikosi vilivyocheza mechi hizo mbili, vina mabadiliko jambo ambalo limeonekana mapema kumbeba Folz ambaye ana miezi miwili tu tangu atambulishwe kuinoa timu hiyo. Mabadiliko ya vikosi hivyo, yameshangaza zaidi kuonekana kwa wachezaji ambao msimu uliopita hawakuwa wakipewa nafasi ya kucheza mechi kubwa mara kwa mara akiwemo nahodha Bakari Mwamnyeto na Aziz Andabwile.

Septemba 16, 2025, Yanga iliipa kipigo Simba cha bao 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Folz alishangaza wengi kwa kuamua kumuanzisha Aziz Andabwile eneo la kiungo mkabaji, na kumweka benchi Balla Moussa Conte ambaye ni usajili mpya. Andabwile akauwasha sana.

Kikosi kilianza hivi; Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Aziz Andabwile, Prince Dube, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua ambaye ndiye alifunga bao.

Baadaye, wakaingia Mohamed Hussein, Mohamed Doumbia, Celestine Ecua, Clement Mzize na Balla Conté waliochukua nafasi za Boka, Abuya, Mudathir, Pacome na Dube.

Hapa kulikuwa na mabadiliko ya wachezaji watatu kutoka kikosi kilichoivaa Simba na Mwamnyeto, Mohamed Doumbia na Clement Mzize walipata nafasi ya kuanza, huku Dickson Job, Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli wakikaa benchi. Lakini Maxi pekee ndiye aliyeingia baadae, huku wenzake hao wakikosakana kabisa.

Kikosi kilikuwa hivi; Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Aziz Andabwile, Clement Mzize, Duke Abuya, Prince Dube, Mohamed Doumbia na Pacome Zouzoua.

Mabadiliko yaliyofanyika, waliingia Mohamed Hussein, Edmund John, Maxi, Celestine Ecua na Moussa Bala Conte.

Baada ya mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, Folz alisema: “Matokeo ni mazuri ingawa siyo kama ambavyo tulistahili, tunahitaji kufanya vizuri zaidi, wakati tunakwenda mapumziko tukiongoza 1-0, niliona haitoshi, lakini nashukuru kwa matokeo haya. Bado tupo kwenye kujenga timu lakini hadi sasa hatupo sehemu mbaya.”

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe alifichua siri, licha ya kikosi chao kukosa muda mwingi wa maandalizi kutoka mchezo wa Ngao ya Jamii na Ligi ya Mabingwa, lakini wanashukuru kupata matokeo mazuri huku hayo yote yakichangiwa na mbinu bora za Folz.

Kamwe alisema, baada ya kukosa muda wa maandalizi mechi iliyopita, wanaamini watakaporudiana na Wiliete wikiendi ijayo, Wanayanga watapata burudani zaidi kwani watajaribu kutumia silaha zao zote.

“Yanga imecheza Dabi ya Kariakoo tarehe 16 kuanzia saa 11 jioni, mechi inaisha kufika saa 3 usiku timu inarejea hotelini, hakuna kulala, wachezaji wanachukua nguo zao moja kwa moja saa 7 usiku wanafika uwanja wa ndege kujiandaa na safari ya kwenda Angola,” alisema Kamwe.

“Alfajiri saa 10 tarehe 17 wachezaji wanasafiri hadi Ethiopia, pale wanapumzika kwa saa tatu, hakuna aliyefunga jicho.

“Wanatoka pale wanaunganisha ndege kuja Angola takribani saa tatu hadi nne angani, wanafika wanapumzika, hakuna aliyefanya mazoezi. Tumepata siku moja tu ya kufanya mazoezi halafu leo (juzi Ijumaa) tumekwenda kwenye mechi kucheza dhidi ya timu ya pili kwa ubora Angola. Tumeitawala karibia kila eneo.

“Tumetengeneza nafasi, tumemiliki mpia na kuwa bora katika kila eneo. Angalia ratiba ilivyobana halafu unaona Yanga inatawala Angola.

“Kinachopikwa na Romain Folz, Mwenyezi Mungu atupe tu uhai mje mshuhudie bomu linalotengenezwa. Pengine kauli ya rais wetu (Hersi Said) aliyosema msimu huu tuna timu bora kuliko miaka yote minne, kwa mtu anayejua mpira ataanza kuona mabadiliko ya kikosi yanayofanyika. Tumecheza ugenini bila ya Dickson Job na hakuna aliyekumbuka kama hayupo, ameingia Bakari Mwamnyeto amecheza na Ibrahim Bacca. Maxi na Mudathir waliocheza Dabi, wamekaa benchi, tumeanza na watu wengine, hakuna aliyezungumza Mudathir yuko wapi wala kwa nini Maxi hakuanza.

“Hapa kati tuna mechi ya ligi (dhidi ya Pamba Jiji itakayochezwa Septemba 24 mwaka hu), halafu hawa Waangola wakija nyumbani ndiyo mechi ambayo Yanga tunakwenda kujaribu kila kitu chetu kwenye Ligi ya Mabingwa.

“Siku hiyo tutakuwa makini sana kwa sababu tunataka kufuzu kwa idadi kubwa ya mabao kwani kuna goli la mama, hapa pekee tumechukua milioni 15, huenda mechi ya marudiano tukaongeza jitihada tukachukua hata milioni 30 za mama, inawezekana. Katika hatua hii ya awali tunataka kukusanya mabao mengi zaidi ili tupate hela nyingi kutoka kwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan,” alisema Kamwe.

Ukiweka kando mechi hizo mbili za kimashindano, Septemba 12 mwaka huu Yanga ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Bandari ya Kenya katika kilele cha Wiki ya Mwananchi na kushinda bao 1-0. Katika mchezo huo, Mzize na Pacome hawakucheza kabisa.

Kikosi kilikuwa hivi; Djigui Diarra, Israel Mwenda, Farid Mussa, Bakari Mwamnyeto, Frank Assinki, Aziz Andabwile, Maxi Nzengeli, Lassine Kouma, Prince Dube, Shekhan Khamis na Celestine Ecua.

Hata hivyo, wakati huu ambao Yanga imekuwa ikifanya vizuri katika mechi mbili za kimashindano ilizocheza, kuna nyota waliosajiliwa dirisha kubwa bado hawajacheza kabisa.

Nyota hao ni Andy Boyeli, Offen Chikola, Frank Assinki, Abubakar Nizar Othuman ‘Ninju’, Abdulnassir Mohamed Abdallah ‘Casemiro’ na Lassine Kouma.