Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tabora, imemuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Bushesha Jimola, baada ya kumkuta na hatia ya kumuua kaka yake, Juma Jimola kwa madai alimdhulumu ng’ombe 10 wa mahari waliotolewa kwa ajili ya binti yake.
Aidha Mahakama hiyo imemuachia huru Maziku Kulwa, maarufu Mgenja aliyekuwa ameshtakiwa na Bushesha, baada ya kumkuta hana hatia katika kesi hiyo ya mauaji.
Miongoni mwa sababu zilizomfanya Bushesha kutiwa hatiani ni pamoja na maelezo yake ya onyo ambayo amenukuliwa akikiri kumuua kaka yake (Juma) baada ya kudai kuwa awali alipanga kumuua na kudai mmoja wa watu waliopewa kazi ya kumuua alimfuata na kumueleza kuhusu mipango ya kaka yake.
Alidai mtu huyo aliyemtaja kwa jina la Mgenja Mkoma, alimweleza amelipwa na Juma (marehemu kwa sasa) Sh800,000 ili atekeleze mauaji hayo ambapo yeye aliwapa ng’ombe wawili wenye thamani ya Sh1.2 milioni ili wakamuue kaka yake (Juma).
Mauaji hayo yalitokea Oktoba 4, 2022 katika eneo la Kadoke, Kata ya Mbutu wilayani Nzega, Tabora ambapo watu watatu walidaiwa kwenda kwa Juma (marehemu kwa sasa),wakamwita pembeni na mmoja wao akampiga na rungu kisha wengine wakamkata kwa panga.
Kesi hiyo ya mauaji ilikuwa ikisikilizwa mbele ya Jaji Frank Mirindo ambaye alitoa hukumu hiyo Septemba 18, 2025 na nakala ya uamuzi huo kupakiwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vilivyotolewa mahakamani hapo Jaji Mirindo alieleza kuwa Bushesha hakuonekana eneo la mauaji ila anahusishwa na mauaji hayo kutokana na jukumu lake la kutafuta wauaji hao ambapo kupitia maelezo yake ya onyo alikiri kuwalipa ng’ombe wawili waliokuwa na thamani ya Sh1.2 milioni ili wamuue kaka yake.
Ilidaiwa Juma alifariki papohapo ambapo mkewe, Banya Malale alijaribu kupiga kelele ila mmoja ya watu hao alimpiga rungu kichwani kisha wakakimbia, ambapo alipoamka aliwapeleka watoto wake kwa shemeji yake, Marko Masunga aliyekuwa akiishi nao jirani.
Washtakiwa hao wawili walishtakiwa kwa mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 ya Kanuni ya Adhabu.
Ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa Bushesha alikodi watu kumuua kaka yake na Maziku alikuwa miongoni mwa watu hao ambaye anadaiwa kuonwa na mke na watoto wa marehemu kuwa ni miongoni mwa waliomshambulia Juma.
Katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulitegemea maelezo ya onyo ya Bushesha ambayo yalipokelewa mahakamani hapo kama kielelezo cha nne.
Sehemu ya maelezo ya onyo ya Bushesha amenukuliwa akieleza kuwa miaka mitatu iliyopita kabla ya mauaji hayo alimuozesha binti yake, Ngolo Bushesha aliyekuwa akiishi kijiji cha Mbutu, wilayani Nzega na kuwa alishirikiana na kaka yake (Juma) katika kumuozesha mtoto wake.
Alidai kuwa walipokea mahari ikiwa ni ng’ombe 10 na baada ya taratibu za harusi kumalizika waliendelea na maisha mengine na siku mbili baada ya harusi, aliamua kurudi nyumbani kwake Kaliua.
Alidai kuwa mwezi mmoja baadaye alirejea Mbutu kwa kaka yake (marehemu kwa sasa) kumuuliza kuhusu ng’ombe hao lakini alikuwa ameshawauza.
Bushesha alieleza kuwa Agosti 2022, akiwa nyumbani kwake, alitembelewa na Mgenja Mkoma aliyekaa muda wa wiki moja, ambapo aliondoka na kurejea Septemba 2022.
Alieleza Mgenja alimweleza kuwa ameenda hapo kwa lengo la kukagua mazingira ya nyumbani anapoishi ili ajipange kwa tukio la mauaji na kuwa alimsikilizisha rekodi ambayo kaka yake (Juma), aliwataka wamuue (mshtakiwa) ili achukue mali zake na walilipwa Sh800,000.
Kupitia maelezo hayo ya onyo, Bushesha alieleza kuwa Mgenja ameamua kumweleza hivyo kwa sababu ameishi naye vizuri ndiyo maana ameshindwa kutekeleza mauaji hayo ambapo kutokana na hilo alimtaka arudi kwa wenzake ili wabadili mpango na kuamua kumuua Juma.
Aidha ushahidi wa mke na mtoto wa marehemu, waliodai kuwatambua washambuliaji wa tukio hilo ambapo mke wa marehemu alidai kumtambua Maziku akiwa amevalia nguo fupi nyeupe huku mtoto wake akidai aliona koti jeupe huku wakitofautiana kuhusu mavazi ya washambuliaji wengine.
Jaji Mirindo amesema mahakama inatathmini iwapo maelezo hayo ya onyo yalichukuliwa kwa mujibu wa sheria na ikiwa ndiyo ushahidi pekee dhidi ya mshtakiwa lazima mahakama iamue iwapo mshtakiwa ameeleza kilichotokea na iwapo maelezo hayo yanathibitisha hatia yake, kwa kiwango cha uhakika kinachohitajika katika kesi ya jinai.
Jaji amesema sehemu ya maelezo hayo ya onyo ya mshtakiwa yameonyesha chuki kati ya Bushesha na kaka yake na kuwa ushahidi huo ulioungwa mkono na mke wa marehemu ambaye alishuhudia tukio la mumewe kuuawa pamoja na shahidi wa tatu (mtoto wa marehemu).
Baada ya uchambuzi wa ushahidi wa pande zote amefikia hitimisho kwamba Maziku hakutambuliwa vya kutosha eneo la mauaji kwani hakutajwa katika maelezo ya onyo na kuwa hakuna ushahidi kuwa Mjenga Mkoma, ndiye Maziku Kulwa hivyo Mahakama hiyo ilimuachia huru.
Kuhusu Bushesha, amesema ni wazi kuwa hakuonekana eneo la mauaji ila anahusishwa na mauaji hayo kutokana na jukumu lake la kutafuta wauaji hao ambapo kupitia maelezo yake ya onyo alikiri kuwalipa ng’ombe wawili waliokuwa na thamani ya Sh1.2 milioni ili wamuue kaka yake.
Jaji amesema ripoti ya uchunguzi wa mwili iliainisha kuwa chanzo cha kifo hicho ni kutokana na kuvuja damu nyingi kulikosababishwa na majeraha mengi kichwani, mkononi na kukatwa mishipa yote ya damu shingoni.
“Huu ni ushahidi wa wazi wa nia ya kusababisha kifo chini ya kifungu cha 200 (a) cha Kanuni ya Adhabu, uthibitisho wa moja kwa moja wa uovu uliofikiriwa hapo awali,”amesema.
Jaji Mirindo alihitimisha kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi ya Bushesha na mahakama hiyo inamtia hatiani na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa chini ya kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu.