Chalamila awapa Ma-DC mbinu ya kutumia gia na AC akiwakabidhi magari

Dar es Salaam. Wakuu wa Wilaya ya Ubungo na Kigamboni wamekabidhiwa magari mapya aina ya Land Cruzer Prado yenye thamani ya Sh200 milioni kila moja huku wakipewa mbinu za namna ya kutumia viyoyozi vyake na gia.

Magari hayo yamekabidhiwa leo Jumatatu Septemba 22, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika hafla iliyofanyika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kabla ya kuwakabidhi magari viongozi hao, Chalamila amesema gari hizo zina kiyoyozi ambacho kitawafaa baada ya kupewa joto na wananchi.

Jingine linalopatikana katika magari hayo, Chalamila ametaja ni kuwa na gia nyingi na kueleza kuwa hazipo kama mapambo bali kuna sehemu zitawaokoa wenyewe na kuna sehemu zitawasaidia kwenda kuwaokoa watu.

Pia gia hizo amesema kazi yake nyingine ni wao watakapokuta maeneo wanayokwenda yana changamoto hadi kufikia hatua ya kutaka kupigwa na wananchi zitawasaidia, kukimbilia haraka kwa OCD (Kamanda wa polisi wa wilaya) kujisalimisha.

“Speed ya haya magari ni kubwa, hivyo mtakapokutana na changamoto yoyote yatawawezesha kukimbia kufika eneo la tukio, au kukimbia pindi unapofikwa na madhila na ndio maana gari hiyo ina gia nyingi kwani imetengenezwa kisasa,” amesema Chalamila.

Hata hivyo ametaka magari hayo yaende kutumika kuleta umoja kati ya wananchi na Serikali na kueleza kuwa katika hilo wana kila sababu ya kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuliwezesha hilo.

“Licha ya kuwa wengine wanasema haina haja ya kumshukuru Rais tunapofanya mambo haya kwa kuwa ni kodi za wananchi, lakini ukweli anapaswa kushukuriwa kwa kuwa hela za kodi haziwezi kufanya kila kitu isipokuwa anahangaika kutafuta hela kila mahali,” amesema Mkuu huyo wa mkoa.

Kwa mujibu wa Chalamila tayari wameshatoa magari ya aina hiyo kwa wilaya nyingine tatu za Kinondoni, Temeke na Ilala.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ameishukuru Serikali kutambua umuhimu wa wakuu wa wilaya kuwa na vitendea kazi.

“Yote haya yanafanywa sio kwa sababu ni starehe au anasa bali ni kuhakikisha tunakwenda kutekeleza wajibu wetu bila kuwepo visingizio vyovyote,” amesema Msando.