Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa Uchaguzi (INEC), imesisitiza msimamo wake kuhusu Luhaga Mpina aliyekuwa akiwania kiti cha urais kupitia chama cha ACT – Wazalendo kwamba hajapitishwa kuwa mgombea wa kiti hicho.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Tume hiyo leo Jumatatu Septemba 22, 2025, INEC imesema ACT – Wazalendo hakina mgombea wa urais na mgombea mwenza wake baada ya kubatilishwa kwa uteuzi wao tangu Septemba 15, 2025 baada ya kuwekewa pingamizi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Tunasisitiza kwamba Chama cha ACT -Wazalendo hakina mgombea urais na mgombea mwenza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa kuzingatia uamuzi wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi wa Tarehe 15 Septemba, 2025 uliotengua uteuzi wa Luhaga Mpina,” imesema taarifa hiyo iliyosaniwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima kwa vyombo vya habari.
Hata hivyo, taarifa hiyo ya INEC imekuja kutokana na taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa Chama cha ACT-Wazalendo jana Jumapili Septemba 21, 2025 kikitaarifu umma kwamba mgombea urais wa chama hicho, Luhaga Mpina ataambatana na mgombea mwenza wake na viongozi wakuu wa chama katika mkutano wa uzinduzi wa Ilani ya chama hicho na kushiriki mkutano wa hadhara katika Jimbo la Segerea, jijini Dar es Salaam.
Lakini INEC imeeleza kutokutambua uwepo wa mkutano huo ikisisitiza taarifa kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo haioneshi uwepo wa mkutano wa ACT – Wazalendo katika eneo ambalo chama hicho kinatangaza kufanya mkutano wake leo.
“Taarifa ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Segerea, ambaye ni mratibu wa kampeni za ubunge, inaonesha kuwa hakuna ratiba ya mkutano wa kampeni za mgombea wa ubunge wa Chama cha ACT – Wazalendo katika eneo lililotajwa na taarifa ya ACT – Wazalendo,” imesema taarifa hiyo.
Kufuatia hatua hiyo, INEC imekitaka Chama cha ACT Wazalendo kuzingatia masharti ya kanuni ya 35 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025 inayohusu utaratibu na ratiba za kampeni za ubunge.
Hata hivyo, Mwananchi imemtafuta mgombea ubunge wa Segerea kwa tiketi ya ACT- Wazalendo, Emmanuel Mvula amesema wamefuata taratibu zote za kuandaa mkutano huo kwa kuwasiliana na waratibu wa INEC.
“Tulifanya mawasiliano yote na INEC na barua za kubadilisha uwanja ziliidhinishwa kwa ajili ya mkutano huu. Mkutano huu unawajumuisha madiwani wote wa Dar es Salaam, lakini ghafla leo tunashangaa… ishu kubwa ni Mpina kuhudhuria.”
“Hii ndio hofu kubwa kwao, lakini chama kimefuata taratibu zote zinazotakiwa kwa ajili ya kufanya mkutano huu. Tuliandika barua ya kubadilisha uwanja ilipokelewa na kufanya uamuzi kwamba tufanye leo mkutano wetu,” amesema Mvula.
INEC yasisitiza kanuni kufuatwa
Kufuatia hatua hiyo, INEC imeitaka ACT Wazalendo kuzingatia masharti ya kanuni ya 35 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025 inayohusu utaratibu na ratiba za kampeni za ubunge.