Kadi nyekundu yamliza Kikoti | Mwanaspoti

KIUNGO mshambuliaji wa Namungo, Lucas Kikoti amezungumzia tukio la kuwa mchezaji wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu msimu huu 2025/26 kuwa amepata kadi hiyo akiwa katika majukumu ya kuipambania timu yake, lakini amesikitika kushindwa kumaliza mchezo.

Kikoti ameingia katika rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu msimu huu baada ya Massoud Abdallah ‘Cabaye’ anayekipiga Tanzania Prisons kufungua msimu uliopita.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kikoti aliyeingia uwanjani katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi akitokea benchini na kushindwa kumaliza mechi, alisema kilichotokea ni sehemu ya mchezo akiwa kwenye majukumu yake kama mchezaji lakini anawaomba msamaha mashabiki wa timu hiyo na kuwapongeza wachezaji wenzake kwa kumaliza dakika 90 wakiibuka na ushindi.

“Nimepata kadi nyekundu nikiwa kwenye majukumu yangu ya kuhakikisha naipambania timu yangu kupata ushindi tulioupata, lakini ninachoumia ni kushindwa kumaliza mchezo licha ya kuingia nikitokea benchini, nawapongeza wachezaji wenzangu kwa kupambana na kuipa timu matokeo,” alisema Kikoti na kuongeza;

“Sitaki kuzungumzia uamuzi ni sahihi au sio sahihi kila mmoja alikuwa kwenye majukumu yake, mwamuzi amefanya kazi yake kama anavyotakiwa kufanya na mimi nimeambulia kile nilichostahili, nawaomba radhi mashabiki wa Namungo, benchi la ufundi na wachezaji wenzangu.”

Kikoti aliyeanzia benchini, aliingia kipindi cha pili na kuonyeshwa kadi za njano mara mbili zilizosababisha atolewe nje ya uwanja kwa kadi nyekundu katika dakika ya 90. Licha ya kadi hiyo Namungo ilimaliza mchezo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.