Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameiomba Jamhuri isihangaike kuwaita mashahidi kuthibitisha baadhi ya vielelezo vya ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili, akisema kuwa hana shida navyo.
Lissu amewasilisha ombi hilo mahakamani baada ya kusomewa shtaka la uhaini linalomkabili na kujibu, kisha akasomewa maelezo ya awali ya kesi hiyo.
“Waheshimiwa majaji, lakini pia kuna vielelezo vya upande wa mashtaka ambavyo sina shida navyo, kwa hiyo upande wa mashtaka wasihangaike tu kuleta mashahidi kuthibitisha hivyo tunapoteza muda bure tu,” amesema Lissu.
Miongoni mwa vielelezo ambavyo Lissu amesema anakubaliana navyo ni ripoti ya mtaalamu wa picha jongefu (video) inayomuonesha Lissu akitamka maneno anayoshtakiwa nayo kuonesha kuwa ni halisi, pamoja na nyaraka za makabidhiano ya video hiyo.
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) James Karayemaha na Ferdnand Kiwonde,
Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025 na kusomewa shtaka hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, lakini hakutakiwa kujibu chochote, kukubali wala kukana kutokana,
Hii ni kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo isipokuwa katika hatua ya uchunguzi wa awali, kabla ya kuhamishiwa Mahakama.
Baada ya upelelezi kukamilika na kuhamishiwa Mahakama Kuu kuwa na mamlaka ya kuisikiliza, leo Septemba 22, 2025 amesomewa shtaka hilo na kujibu.
Alipoulizwa kama ni kweli au si kweli, Lissu katika majibu yake, kwanza amekiri kutamka maneno hayo yaliyonukuliwa kwenye hati ya mashtaka yanayodaiwa kuwa yanaunda kosa la uhaini, lakini akasema kuwa maneno hayo hayaoneshi kosa lolote la uhaini.
Badala yake, amesema yanaonesha kwamba yeye ni mpinzani tu wa Serikali na mpinzani wa uchaguzi na alitaka kuzuia uchaguzi hivyo kosa hilo si la kweli.
Lissu baada ya kujibu shtaka hilo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawabu Issa amemsomea maelezo ya awali ya kesi hiyo, kisha akatakiwa kubainisha mambo anayokubaliana nayo na asiyokubaliana nayo.
Miongoni mwa mambo aliyokubaliana nayo katika maelezo hayo ni majina yake kamili, makazi yake, wadhifa wake ndani ya Chadema kuwa Mwenyekiti Taifa wa Chadema, Wakili wa Mahakama Kuu na pia mwanasheria.
Mengine ni shtaka linalomkabili kuwa anashtakiwa kwa kosa la uhaini, kuwa na utii kwa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na pia ana hati ya kusafiria (Passport) iliyotolewa na Idara ya Uhamiaji.
Vilevile Lissu amekubaliana na maelezo kuwa, alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa( JKT) kikosi cha 841KJ Mafinga mwaka 1989 na kumalizia kikosi cha 844 KJ Itende, kilichopo Mbeya.
Hata hivyo, alitoa tahadhari kuwa kuhudhuria mafunzo hayo kusichukuliwe kama yeye ni mwanajeshi, huku akidai anajua ushahidi wa upande wa mashtaka kuhusiana na hoja hiyo.
Maelezo mengi ambayo Lissu amekubaliana nayo ni kuwa alikamatwa Aprili 9, 2025 wilayani Mbinga na kurejeshwa Dar es Salaam, siku iliyofuata alipelewa mahakamani na kufunguliwa shtaka la uhaini.
Baada ya kubainisha mambo hayo anayokubaliana nayo, Mahakama imeandaa hati ya hoja zinazobishaniwa ambazo zimesainiwa na pande zote, yaani upande wa mashtaka, mshtakiwa na Mahakama.
Ni hoja hizo ndizo ambazo upande wa mashtaka utajikita katika ushahidi wake kuzithibitisha kupitia mashahidi wake watakaowaita.
Upande wa mashtaka umeieleza Mahakama kuwa na mashahidi 30 wakiwamo maofisa wa Jeshi la Polisi na wengine raia ambao hata hivyo Mahakama ilitoa amri ya kuwalinda.
Ulinzi huo unahusu kutotajwa majina yao wala taarifa zozote zinazoweza kufanya wakatambulika wao, familia zao na watu wengine wa karibu yao, kutokuonekana wakati wakitoa ushahidi wao na kutumia majina bandia.
Baada ya upande wa mashtaka kutaja idadi ya mashahidi wake, Lissu alidai kuwa anatarajia kuwa na mashahidi 15, lakini hakuwa na vielelezo.
“Mheshimiwa majaji natarajia kuwa na mashahidi 15, lakini sitakuwa na vielelezo,” amedai Lissu.
Amewataja mashahidi wake hao kuwa ni Samia Suluhu Hassan aliyedai kuwa ana anuani mbili, moja ipo Ikulu Chamwino Dodoma na nyingine ni Ikulu ya Magogoni Kivukoni, jijini Dar es Salaam.
Wengine ni Dk Philip Mpango, amedai anapatikna Ofisi ya Makamu wa Rais, Mji Mkuu wa Serikali Mtumba, pia yupo Kassim Majaliwa, ambaye anuani yake inasomeka yupo Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma.
Shahidi wa nne wa Lissu amemtaja Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillius Wambura; Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) Ramadhani Kingai.
Pia, yupo Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa na Ujasusi, ambaye Lissu amedai kuwa hamfahamu jina lake, pamoja na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ramadhani Ng’anzi.
Pia, wapo wana harakati kutoka Uganda na Kenya ambao ni Agatha Atuhaire kutoka Uganda, Boniface Mwangi(Kenya), Dk Willy Mutunga (Kenya) na Martha Karua kutoka Kenya.
Wengine ni Mkurugenzi wa Jambo TV, John Marwa, Naibu Katibu Mkuu Chadema ( Aman Golugwa), Makamu Mwenyekiti cha Chadema (John Heche) na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.
Mahakama hiyo imewarekodi mashahidi wote hao aliowataja kwa ajili ya taratibu za uandaaji wa hati za wito wa kufika mahakamani pale muda utakapofika, kwa mujibu wa sheria.
Baada ya ratatibu hizo za usikilizwaji huo wa awali kukamilka kesi hiyo imepangwa kuanza usikilizwaji rasmi, Oktoba 6, 2025, Jamhuri itaanza kutoa ushahidi wake kuthibitisha shtaka hilo, kabla ya Lissu kujitetea iwapo Mahakama itamuona kuwa ana kesi ya kujibu baada ya Jamhuri kufunga ushahidi wake.