Mahakama Kuu kuamua hatima ya Tundu Lissu, leo

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, leo Jumatatu Septemba 22, 2025, inatarajia kutoa uamuzi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema taifa, Tundu Lissu.

Hatua hiyo inatokana na pingamizi lililowasilishwa na mshtakiwa huyo mahakama hapo Septemba 16, 2025 la kudai kuwa hati ya mashtaka ni batili kutokana na kukiuka masharti ya sheria.

Uamuzi huo unatarajia kutolewa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) James Karayemaha na Ferdnand Kiwonde, wanaosikiliza kesi hiyo.

Mwenyekiti wa Chadema taifa, Tundu Lissu.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Septemba 16, 2925 baada ya kusomewa shtaka hilo Mahakama Kuu, Lissu kabla ya kujibu shtaka, kukubali au kukana aliieleza Mahakama hiyo kwanza, kwenye vifungu vya 294 (1) na 295(1) vya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) Marekebisho ya mwaka 2023

Alidai kuwa kwa mujibu wa vifungu hivyo hawezi kujibu shtaka hilo kwani ana pingamizi dhidi ya uhalali wa hati ya mashtaka, mpaka litakapoamuliwa.

Lissu amedai kuwa hati hiyo haionyeshi kosa lolote na hasa la uhaini.

Alieleza kuwa msingi wa pingamizi lake hilo uko katika kifungu cha 135 cha CPA, ambacho kinaeleza kuwa kila hati ya mashtaka inapaswa kuwa na maelezo ya kosa analoshtakiwa nalo mshtakiwa na taarifa za msingi zinazotosheleza kuonesha asili ya kosa analotuhumiwa.

Alidai kuwa hati ya mashtaka isipokuwa na taarifa hizo ni batili kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Akizungumzia hati ya mashtaka ya kesi yake, Lissu alidai kuwa hati ya mashtaka aliyosomewa  alipopandishwa kizimbani, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, Kisutu na  aliyopewa Agosti 18, 2025, kesi hiyo ilipohamishiwa Mahakama Kuu zinatofautiana.

Hata hivyo aliendelea kudai kuwa kwenye hati za mashtaka zote, hakuna kosa la uhaini wala jinai kwa mujibu wa sheria za Tanzania hivyo ziko kinyume na masharti ya kifungu cha 135 cha CPA.

Akifafanua kasoro za hati hiyo ya mashtaka, Lissu alirejea kifungu cha 39(2) (d) cha PC anachoshtakiwa nacho. Kifungu hicho kinaeleza kuwa;

(2) Mtu yeyote ambaye, yumo katika ndani ya Jamhuri ya Muungano, akiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano au popote, anajenga nia kusababisha au kuwezesha kusababishwa, au anajenga nia ya kuchochea, anashawishi, shauri au kuusia mtu yeyote au kikundi cha watu kusababisha au kuwezesha kusababishwa yoyote kati ya matendo au malengo yafuatayo:

‎(d) kutishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Bunge na Mahakama ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, na kubainisha nia hiyo kwa kuchapisha maandishi au machapisho au kwa  kitendo chochote cha siri kinachojionyesha cha hali yoyote, atakuwa na  hatia ya kosa na atawajibika kwa adhabu ya kifo.

Alidai kesi yake hiyo si ya kwanza ya uhaini nchini bali ni ya tatu na kwamba hivyo kuna mwongozo wa namna ya kuendesha shtaka la ugaidi.

Lissu alidai kuwa nia ya uhaini lazima ionekane kwa kuchapisha au kwa matendo na kwamba katika kesi yake maelezo ya kosa yanaeleza kuwa alionesha nia ya uhaini kwa kutamka, huku akidai kuwa maneno matupu kwa mujibu wa kesi ya Hatibu Gandhi hayatengenezi uhaini isipokuwa kama yanaelezea uhaini.

Vile vile alidai kuwa kwa mujibu wa kesi hiyo maneno ya mtu mmoja hayawezi yakawa uhaini, huku akirejea neno mojamoja kati ya maneno anayodaiwa kuyatamka na kutoa maana yake kwa mujibu wa kamusi.

Alihoji ni wapi kuna uhaini katika maneno hayo huku pia akidai kuwa hakuna mahali ambako ameitaja Serikali na vyombo vyake, Bunge, Mahakama wala viongozi wake.

Hivyo alisema kuwa ndio maana amewaita Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa mashahidi wake na wengine watafuata.

Akijibu pingamizi hilo, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, kwanza aliomba Mahakama hiyo itupilie mbali pingamizi hilo kwa madai mshtakiwa huyo hajaonyesha  sehemu gani zenye kasoro.

Katuga alidai kuwa kama hati hiyo ya mashtaka ilikuwa na mapungufu, mshtakiwa alitakiwa abainishe mapungufu hayo kwa kuyaorodhesha, lakini hakufanya hilo, hivyo hana sifa za kupinga.

Katuga alidai kuwa hati ya mashtaka haina mapungufu yoyote kwa kuwa imejengwa chini ya kifungu 138 cha CPA, ambacho alidai kuwa hakiruhusu kuweka pingamizi katika hatua hii ya usikilizwaji wa awali.

Alidai kuwa kifungu hicho138a kinaeleza jinsi hati ya mashtaka itakavyokuwa na 138(a) (i) kinasema hati ya mashtaka lazima ianze na maelezo ya kosa na kinaeleza wazi kwenye maelezo ya kosa 138a (2) inaeleza lazima iandikwe kwa lugha ya kawaida ili kuepuka  ‘technical tense’.

Alifafanua kuwa kifungu hicho 138(a) kinaeleza jinsi hati ya mashtaka itakavyokuwa na 138(a)(1) kinasema hati ya mashtaka lazima ianze na maelezo ya kosa na kinaeleza wazi kwenye maelezo ya kosa 138a (2) inaeleza lazima iandikwe kwa lugha ya kawaida ili kuepuka kutumia lugha ya kitaalamu.

Kuhusu kifungu cha 39(2)d cha Sheria ya Kanuni ya adhabu kilichofanyiwa marejeo mwaka 2022 ambacho ndicho mshtakiwa anashtakiwa nacho, Katuga alidai kuwa kinachambua viini ambavyo vinajenga kosa.

Kuhusu hoja ya Lissu kuwa kuzuia uchaguzi haijaelezwa kuwa ni kosa la uhaini, Katuga alijibu kuwa yeye anashtakiwa kwa nia ya kutengeneza nia na kudhihirisha kwa  kuchapisha hiyo taarifa kwa lengo la kuitishia Serikali.

Kuhusu, madai ya Lissu kuwa hakuna sehemu kwenye  maneno amemtaja raisi, makamu wa raisi wala waziri mkuu na hiyo taarifa ya hati ya mashtaka hayana uhaini, Katuga alijibu kuwa suala la kuwataja na kutowataja viongozi hao ni suala la ushahidi.

Kuhusu tofauti ya hati ya mashtaka aliyosomewa katika Mahakama ya Kisutu na aliyosomewa Mahakama Kuu, Wakili Katuga, alidai kuwa hati ya mashtaka iliyosomewa kwenye maelezo ya mashahidi na vielelezo ni ile iliyosajiliwa Mahakama Kuu na ndio taarifa ambayo Mahakama Kuu ina mamlaka ya kutolewa marekebisho kwa mujibu wa kifungu 263.

Katuga alifafanua kuwa baada ya upelelezi wa kesi kukamilika, DPP huandaa taarifa ikiwemo hati ya mashtaka na kuipelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusajiliwa.

Alidai baada ya kusajili taarifa hiyo, ndipo hurejeshwa mahakama ya chini kwa ajili ya kusomwa commital  na hiyo ni kwa mujibu wa kifungu 263 cha CPA.

“Kifungu 262(6) CPA kinaeleza kuwa DPP atakapojiridhisha ushahidi unaojitosheleza ataandaa taarifa na hati ya mashtaka na kuwasilisha Mahakama Kuu na maelezo ya mashahidi wanaotarajia kuitwa na hiki kifungu ni kwa ajili ya kesi zinazosikilizwa Mahakama Kuu” alidai Katuga.