……………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania ipo tayari kufanya kazi kwa karibu na jumuiya ya wafanyabiashara wa Marekani pamoja na kuwezesha uwekezaji kupitia sheria zilizofanyiwa marekebisho, miundombinu iliyoboreshwa, na uchumi huria.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani lililofanyika kando ya Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 80) Jijini New York nchini Marekan Amesema Serikali ya Tanzania inatambua sekta binafsi ni mshirika mkuu katika juhudi za maendeleo kwa ajili ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imekuwa na utulivu wa kisiasa na kijamii kwa miaka 60, miundombinu inayoboreshwa kwa kasi huku mazingira ya biashara yakiwa yameboreshwa kwa kiasi kikubwa hivyo wafanyabiashara na wawekezaji wa Marekani wanaweza kutumia fursa hiyo kuwekeza Pia ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania kufikiria na kuchukua hatua kimataifa, kwa kuchangamkia fursa zilizopo katika soko la Marekani.
Ameongeza kwamba Serikali ya Tanzania inafanya kazi kila mara ili kuboresha na kuweka mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji.
Amesema kwa sasa imepunguza muda wa usajili wa biashara kutoka siku 14 hadi saa 24, Vibali vya uwekezaji vilivyokuwa vikichukua miezi, sasa vinachukua saa au siku kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA).
Amesema Serikali imedhamiria kuboresha mazingira ya Udhibiti, ikiwa ni pamoja na kuondoa kanuni zisizo za lazima pamoja na kuwekeza katika elimu ili kuzalisha wafanyakazi wenye ujuzi unaohitajika.
Makamu wa Rais amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza nchini Tanzania katika sekta muhimu na za kimkakati ikiwemo madini adimu na muhimu ambayo ni chachu ya mapinduzi ya kijani.
Amesema, wakati Marekani inawekeza kwenye nishati safi, Tanzania inasimama kama mtoaji wa kuaminika wa nyenzo zinazohitajika kama vile madini ya Graphite yaliyopo Mahenge, mkoani Morogoro ambayo yanakadiriwa wa kutoa hadi asilimia 15 ya mahitaji ya betri duniani.
Ametaja pia uwepo wa madini ya nikeli ya Kabanga, pamoja na lithium ambayo ni miongoni mwa amana kubwa zaidi za viwango vya juu duniani.m
Amesema uwekezaji katika madini unasisitiza zaidi katika uongezaji thamani kuanzia uchimbaji madini, usindikaji hadi uzalishaji wa kiwango cha betri.
Aidha, Makamu wa Rais ametaja fursa zilizopo nchini Tanzania katika sekta ya kidijitali ambapo amesema mabadiliko mazuri ya kidijitali ambayo yamefanyika nchini Tanzania, ni dalili ya uwezo mkubwa uliopo.
Ameongeza kwamba, kuongezeka kwa matumizi ya mtandao kutoka asilimia 13 hadi asilimia 60 katika miaka mitano,miamala ya pesa kwa simu imefikia dola bilioni 75- karibu na asilimia 90 ya Pato la Taifa na kuna takriban akaunti milioni 27 za pesa kwa watu milioni 65 pamoja na mapinduzi ya Kampuni za Tanzania kama vile NALA,ambayo kwa sasa inahudumia watumiaji zaidi ya laki tano duniani kote katika miamala ya kifedha.
Vilevile, Makamu wa Rais amewakaribisha kuwekeza katika sekta zingine kama vile Kilimo ambapo Tanzania inajivunia kuwa na hekta milioni 44 za ardhi inayofaa kwa kilimo. Amesema Tanzania inahitaji washirika katika kilimo janja, kikiwemo kilimo cha usahihi, teknolojia ya ndege zisizo na rubani, kilimo kinachoendeshwa na Akili Unde na uwekezaji katika maeneo ya usindikaji wa mazao ya kilimo.
Halikadhalika, Makamu wa Rais ametaja fursa zilizopo katika huduma za Afya kama vile kushirikiana na Makampuni ya Marekani katika kutengeneza dawa na vifaa tiba kwa ajili ya watu wa Afrika Mashariki wapatao milioni 300 na watu bilioni 1.4 chini ya Eneo huru la Biashara Barani Afrika.
Amesema ipo fursa katika sekta ya miundombinu ambapo, baada ya kukamilika kwa Reli ya Kisasa (SGR) yenye urefu wa kilomita 2,561 itabeba abiria na tani 10,000 za mizigo kwa kila treni ikiunganisha Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda.
Vilevile fursa zinazotolewa na sekta ya utalii ikiwa Tanzania inakaribisha wageni zaidi ya milioni 2 kila mwaka, na kuingiza mapato ya dola bilioni 3.37.
Katika Jukwaa hilo, Makamu wa Rais amebainisha Tanzania inahitaji kuvutia jumla ya dola za Marekani bilioni 185 katika kipindi cha miaka 5 ijayo, sawa na dola za Marekani bilioni 37 kila mwaka ili kuiwezesha Tanzania kufikia malengo makuu ya Dira 2050 katika kipindi cha kati ikiwemo kujenga nchi ya viwanda, miundombinu fungamanishi na biashara imara.
Uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na Tanzania umejikita kwenye biashara na uwekezaji, huku Marekani ikiwa mshirika mkubwa wa Tanzania katika sekta za afya, kilimo na miundombinu.
Biashara ya bidhaa baina ya nchi hizi mbili kwa jumla imeongezeka kutoka dola milioni 228 mwaka 2020 hadi dola milioni 770 mwaka 2024.
Marekani imeendelea kuwa muuzaji bidhaa kwa Tanzania, na kufikia dola milioni 566 mwaka 2024, wakati mauzo ya Tanzania kwenda Marekani yaliongezeka kutoka dola milioni 47 mwaka 2020 hadi dola milioni 204 mwaka 2024.
Uwekezaji wa mitaji wa moja kwa moja kwa mwaka kutoka nchini Marekani umeongezeka kutoka dola milioni 12.3 mwaka 2020 hadi dola milioni 40 mwaka 2023, huku uwekezaji wa jumla wa mitaji ukifikia dola bilioni 1.
Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani limehudhuriwa na wawekezaji na wafanyabiahsara kutoka Tanzania na Marekani ambapo wameipongeza Tanzania kwa uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji pamoja na kuwa na sera zinazotabirika, amani na wananchi wakarimu. Pia wawekezaji wa Marekani wamesema malengo ya Dira 2050 yakufikia uchumi wa dola Trilioni 1 yanawezekana kutoka na fursa mbalimbali zilizopo.