Malale apata kianzio Ligi Kuu Bara

USHINDI wa bao 1-0 iliyopata Mbeya City dhidi ya Fountain Gate ikicheza ugenini, umempa pawa kocha wa timu hiyo, Malale Hamsini aliyesema amepata kianzio Ligi Kuu Bara inayoendelea kushika kasi ikiingia raundi ya pili kwa sasa.

Mbeya City iliyorejea Ligi Kuu baada ya kupanda daraja ilipata ushindi huo kwa bao la penalti iliyopigwa na Habib Kyombo na kuipa pointi tatu muhimu ugenini na kocha Malale alisema huo ni mwanzo mzuri kwa mechi nyingine zilizopo mbele yao ikiwamo ya Azam FC.

Akizungumza na Mwanaspoti, Malale alisema ushindi huo umempa nguvu sana ni kuona anaanza vyema na tuna matumaini makubwa ya msimu huu.

Malale alisema ni wazi mastaa waliosajiliwa wanatambua kilichowapeleka, lakini ari yao ni kubwa kuhakikisha kwa pamoja wanarejesha heshima ya Mbeya.

“Hatua ya kuanza kupata ushindi ugenini imewapa nguvu kubwa na sasa tunataka kuendeleza ushindi zaidi, sio rahisi kupata pointi tatu ugenini lakini tulijua udhaifu wa wapinzani wetu na tukawaadhibu.

“Wachezaji wangu kwa sasa wamesahau matokeo hayo haraka ili waanze kujipanga juu ya mchezo ujao, kwani wakiendelea kufurahia wataanguka kutokana na kujiamini wanaweza kuwafunga watakaokuja,” alisema Malale anayejiandaa kukabiliana na Azam iliyotoka kushinda 2-0 ugenini katika Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya El Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini.

Timu hizo hivi karibuni zilivaana katika tamasha la Mbeya City lililofanyika Septemba 6 na Azam kushinda kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya na mechi ya keshokutwa zitacheza mechi hiyo ya Ligi kuanzia saa 3:00 usiku.