Moto wateketeza ghorofa Kariakoo, wafanyabiashara wahaha

Dar es Salaam. Moto mkubwa uliozuka leo Jumatatu Septemba 22, 2025, katika jengo la ghorofa saba lililopo Mtaa wa Narung’ombe, Kariakoo, umesababisha taharuki kubwa miongoni mwa wafanyabiashara na wamiliki wa stoo zilizohifadhi bidhaa mbalimbali.

Moto huo ulianza saa 10 jioni baada ya wafanyabiashara kushuhudia moshi ukitokea katika ghorofa lililokuwa na shehena ya bidhaa.

Miongoni mwa walioathirika moja kwa moja ni mmiliki wa moja ya stoo katika jengo hilo, ambaye jina lake halikupatikana mara moja. Mwanamke huyo alionekana akihaha huku akisimama na kukaa kila mara aliposhuhudia magari ya Zimamoto na Uokoaji yakipambana na moto huo.

Kwa majonzi makubwa alisikika akisema; “Utasikia jana ulilala tajiri, unaamka masikini, ndiyo hivi sasa. Mungu wangu tusaidie.”

Amesema mbali na stoo yake kuungua, pia anamiliki duka la viatu katika jengo jingine lililopakana na eneo lililoungua, huku dada yake akiwa na stoo ya viatu na nguo katika ghorofa ya sita ya jengo hilo.

“Stoo iliyoungua nimekubali kupata hasara, lakini hofu yangu ni kwamba moto unaweza kusambaa na kushika duka lingine lililobaki. Nikifikiria hilo najiona kuchanganyikiwa zaidi,” alisikika akilalama.

Mwanamke huyo pia amekiri kuwa tukio hilo limekuwa funzo kwake kwa kutokuwa na bima ya biashara, kama ilivyo kwa wafanyabiashara wengi wa Kariakoo.

“Sijawahi kufikiria bima kwa sababu sikuwahi kukumbwa na majanga, lakini sasa nimepata funzo. Hata sijui nini kimesababisha moto, maana stoo yangu ipo jirani na chumba kinachotumika kwa ibada,” aliendelea kulalama


Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK), Donut Kibwana amesema ajali hiyo imezua taharuki kubwa na kuathiri shughuli za kibiashara katikaeneo hilo.

Amesisitiza mshikamano wa wafanyabiashara na wamiliki wa majengo katika kukabiliana na majanga ya aina hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kibwana amesema moto ulianzia ghorofa ya tano na kusambaa haraka kutokana na bidhaa zilizohifadhiwa humo kuwa rahisi kushika moto.

Amebainisha kuwa changamoto kubwa imekuwa ni magari ya Zimamoto kuchelewa kufika eneo la tukio kwa sababu ya barabara kuzibwa na biashara za wamachinga.

“Moto ulianzia juu na ukawa unaruka flow moja kwenda nyingine. Bidhaa nyingi zimeteketea, na muda ulipotea kwa sababu magari ya zimamoto yalichelewa kufika hadi wafanyabiashara wadogo walipoondoa biashara zao kufungua njia,” amesema.

Ajali za moto Kariakoo zazidi kuongezeka

Kibwana amesema tukio la leo linaongeza orodha ya majanga ya moto yaliyowahi kutokea katika eneo la Kariakoo ndani ya muda mfupi, akitolea mfano jengo la DDC lililoungua hivi karibuni.

“Baada ya tukio hili, tutaharakisha kikao cha wadau kujadili kwa kina namna ya kuimarisha usalama, maana leo ni ghorofa hii, kesho inaweza kuwa janga kubwa zaidi,” amesema.

Aidha, Kibwana ameeleza kuwa baadhi ya ajali hizo zimekuwa zikihusishwa na matatizo ya mifumo ya umeme, hivyo Jumuiya ya Wafanyabiashara ikishirikiana na mamlaka husika itaharakisha ukaguzi wa majengo yote ya biashara.

“Tunapaswa kuchukua hatua za haraka. Hatuwezi kuendelea kushuhudia majengo yanaungua mara kwa mara. Lazima tuimarishe mifumo ya usalama na kushirikiana kwa karibu na mamlaka husika,” amesema.