Moto wateketeza stoo ya viatu Kariakoo

Dar es Salaam. Taharuki imetanda katika Mtaa wa Narung’ombe, Kariakoo baada ya sehemu ya jengo lenye ghorofa saba kuungua moto leo, huku chanzo cha moto kikiwa bado hakijajulikana.

Moto huo umetokea leo Septemba 22, 2025 katika Mtaa wa Narung’ombe katika moja ya ghorofa linalotumika kuhifadhia mizigo ya wafanyabiashara mbalimbali waliopanga eneo la Kariakoo.

Mashuhuda wamesema moto ulianza saa 10 jioni katika ghorofa la tano la jengo hilo, ambalo linalotumika kwa biashara ya viatu, huku sakafu za chini zikiwa na maduka mbalimbali ya rejareja na jumla.

“Nilikuwa natoka msikitini nimefika hapa ghafla nikaanza kuona moshi mzito ukitoka katika ghorofa ya tano, sekunde chache baadaye watu wakaanza kupiga kelele ‘moto, moto!,” amesema Mohamed Ali, mfanyakazi wa eneo hilo.

Shuhuda mwingine, Mariam Seif, ambaye duka lake lipo jirani na jengo hilo, amesema kuwa siku mbili zilizopita mmoja wa wafanyabiashara aliingiza mzigo wa viatu kwenye jengo hilo.

“Huyu jamaa ameleta mzigo mkubwa wa viatu, sijui leo ndiyo moto umetokea. Hatujui kama mizigo yake yote imeteketea, lakini moto ulipoanza ulikuwa mkali sana,” amesema Mariam.

Kwa mujibu wa mashuhuda, juhudi za kuzima moto zilianza kwa wananchi kutumia vizima moto vidogo kabla ya magari ya zimamoto kufika eneo la tukio.

Hata hivyo, kutokana na ukubwa wa jengo na bidhaa zilizokuwa zikihifadhiwa humo, moshi ulioongezeka  na kusababisha hofu kwa wafanyabiashara wengine waliokuwa na bidhaa ndani ya jengo hilo.

“Changamoto ni kwamba humo ndani kuna bidhaa nyingi ambazo zinashika moto haraka, hasa viatu vya plastiki na ngozi. Hivyo moto ulipoanza, ulisambaa kwa haraka sana,” Omari Hamisi ambaye ni mfanyabiashara.