Mwenyekiti mstaafu CCM Moshi Mjini, Alhaj  Shamba Afariki dunia

Moshi. Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini, Alhaj Omar Shamba, amefariki dunia ghafla leo Septemba 22, 2025 akiwa nyumbani kwake.

Alhaj Shamba aliwahi kuhudumu kama Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017 hadi 2022, ambapo alishindwa kutetea nafasi hiyo na   kuchukuliwa na Mwenyekiti wa sasa, Faraj Swai.

Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Moshi Mjini, Athuman Ally, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho   na kueleza kuwa marehemu amefariki leo Septemba 22, saa tano asubuhi.

“Ni kweli Mzee wetu Shamba amefariki nyumbani kwake leo saa tano asubuhi. Jana alikuwa msibani na pia alihudhuria swala msikitini, lakini ghafla leo akafariki. Tutatoa taarifa zaidi baada ya kufika nyumbani kwake jioni hii,” amesema Ally.

Akizungumzia msiba huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, amesema chama kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mzee Shamba, hasa katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu.

“Shamba alikuwa ni mtu mzuri, mchapakazi na mwenye msimamo. Kabla ya kuwa mwenyekiti, aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Njoro kwa miaka mitano na alifanya kazi kubwa kwa maendeleo ya kata hiyo,” amesema Boisafi.

Aidha, ameongeza kuwa enzi za uongozi wake, CCM Moshi Mjini ilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa ubunge mwaka 2020, ushindi ambao haukuwa umepatikana kwa zaidi ya miaka 25 tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi.

“Mzee Shamba alikuwa mtu mwenye imani, msimamo na asiye na tamaa. Mara zote alikuwa tayari kupambana hadi mwisho kwa jambo aliloamini. Tumempoteza kiongozi na mshauri muhimu kwa chama na jamii,” ameongeza.

Amesema ratiba ya mazishi na shughuli nyingine zitatangazwa baadaye