NIT KUCHANGIA MILIONI MBILI BONANZA LA MIAKA 50 YA CHUO HICHO

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv 

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, ameahidi kuchangia kiasi cha Shilingi milioni mbili kwa ajili ya bonanza la michezo na maandalizi ya sherehe za baada ya maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho.

Akizungumza leo Septemba 22, 2025 wakati wa uzinduzi wa bonanza hilo ulifanyika  chuoni hapo Dkt. Mgaya amesema mchango huo unalenga kuongeza ufanisi wa shughuli hizo na kuandaa sherehe zenye mvuto baada ya maadhimisho hayo.

“Leo tunaposherehekea historia hii, tunatumia bonanza hili si kwa burudani pekee, bali pia kama sehemu ya kuimarisha mshikamano, ushirikiano na afya zetu, ili kuongeza ari ya utendaji miongoni mwa watumishi na jamii ya NIT,” amesema.

Aidha, ameongeza kuwa afya bora ya watumishi ni nguzo muhimu ya utendaji bora na msingi wa mafanikio ya taasisi.

Bonanza hilo liliambatana na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, pete, wavu, kikapu, kuvuta kamba, kufukuza kuku, kukimbia magunia na riadha.

Dkt.  Mgaya amesema kutokana na matokeo chanya ya ushiriki wa mazoezi kwa watumishi, ofisi yake itaendelea kushirikiana na mtaalamu wa mazoezi kwa ajili ya kutoa elimu hiyo chuoni na kwa jamii pana ili kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara.

“Naomba kutumia jukwaa hili kuwasihi watumishi wote tushiriki kwa wingi katika mazoezi yanayoratibiwa na Ofisi ya Naibu Mkuu wa Chuo – Utawala na Fedha, ili kudumisha afya zetu,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bonanza, Cornelio Swai, amesema licha ya changamoto za mwingiliano wa ratiba na ufinyu wa bajeti, bonanza hilo limefanikiwa kuvutia ushiriki kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Naye Makamu wa Chuo, Dkt..John John, amesema timu zote zimejiandaa vyema kwa michezo hiyo kutokana na kutambua umuhimu wa mazoezi kwa afya na ustawi wa binadamu.