NMB kukopesha zaidi ya Sh. Bilioni 500 kwa biashara, kilimo, viwanda na madini

Na Mwandishi Wetu, MBEYA.

BENKI ya NMB imesema kuwa kwa sasa ina uwezo wa kumkopesha mteja mmoja zaidi ya Sh. Bilioni 500 kwa ajili ya uendeshaji wa biashara na shughuli zingine za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo, viwanda na uchimbaji wa madini kutokana na kuwa na mtaji mkubwa.

Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB, Alex Mgeni aliyasema hayo juzi jijini Mbeya wakati wa chakula cha jioni na wafanyabiashara wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu  ambao ni wateja wakubwa wa benki hiyo.

Alisema lengo la kutoa mikopo hiyo ni kukuza shughuli za wateja wake na kwamba mikopo hiyo inatolewa kwa kutumia masuluhisho  mbalimbali yaliyoanzishwa na benki hiyo kulingana na kiwango ambacho mteja anataka.

Aidha, Alex aliwahimiza wateja kuendelea kutumia huduma za kimtandao za Benki hiyo ikiwa ni pamoja na matumizi ya NMB mkononi na Benki Mtandao (internet Banking).

“Hizi huduma za NMB mkononi na Internet banking, zinalenga kumpunguzia mteja muda na gharama za kwenda kwenye matawi yetu,” alisema Mgeni.

Alisema benki hiyo kwa sasa imeanzisha mkopo kwa ajili ya Nishati safi ya kupikia kwa wafanyabiashara ambao riba yake ni asilimia moja kwa mwezi na asilimia 12 kwa mwaka.

Mkuu wa Kitengo cha Kilimo wa NMB, Nsolo Mlozi alisema asilimia kubwa ya wateja wa benki hiyo walioko kwenye mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu shughuli zao huwa zinahusiana Zaidi ya mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo.

Alisema baadhi huwa wanakopa kwa ajili ya kununua mitambo ya kilimo, magari ya kusafirishia mazao, kununua mazao na baadhi huwa wanakopa kwa ajili ya kununua pembejeo za kilimo.

Alisema katika ukanda huo kuna baadhi ya mazao ya chakula yamebadilika na kuwa ya biashara kutokana na wakulima kuongeza uzalishaji ikiwemo viazi na mpunga kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji.

“Lakini pia tunakusudia kuanza kutoa mikopo kwa ajili ya mitambo ya umwagiliaji kwa lengo la kuongeza tija kwenye kilimo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Mlozi.

Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Wogofya Mfalamagoha alisema kwa sasa benki hiyo ndiyo kubwa kuliko benki zote nchini akidai kuwa ina matawi katika kila wilaya na mawakala mpaka maeneo ya vijijini.

Alisema kwa mika wiwili iliyopita benki ilikuwa na mawakala 20,000 lakini kwa sasa ina mawakala 60,000 ambao wamesambaa nchi nzima na hivyo akawashauri wananchi kuendelea kuiamini na kuchangamkia huduma inazotoa.

Baadhi ya wateja waliohudhuria hafla hiyio waliendelea kuipongeza Benki ya NMB kwa mafanikio makubwa na kwa namna ambayo imekuwa karibu a biasharta zao na hata kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo yao ya kiuchumi.

Mmoja wa wateja hao, Mhandisi Ralph Makundi alisema mikoppo kutoak Benki ya NMB imempa uwezo wa kufanya kandarasi kubwa na kumjengea uwezo wa kufanya kazi kubwa katika miundombinu ya nchi.

Alisema yeye ni miongoni mwa watu walionufaika na benki hiyo akieleza kuwa wakati anaanza kukopa Kampuni yake ya ujenzi ilikuwa ya daraja la sita lakini kwa sasa iko daraja la kwanza.