Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amekabidhi magari mawili aina ya Land Cruiser Prado kwa Wakuu wa Wilaya ya Ubungo na Kigamboni yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuwawezesha kuwafikia wananchi na kuboresha utoaji wa huduma.
Aidha, katika tukio hilo lililofanyika katika Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, RC Chalamila pia alimkabidhi mlinda mlango wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Yakoub Suleiman, gari aina ya Toyota Crown, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa kutokana na mchango mkubwa wa kipa huyo katika mashindano ya CHAN, licha ya Taifa Stars kutolewa katika hatua ya robo fainali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Chalamila alisema magari hayo yametolewa kwa maelekezo ya Rais Dkt. Samia ili kusaidia katika kuboresha utendaji kazi wa viongozi wa wilaya na kuimarisha huduma kwa wananchi.
“Mheshimiwa Rais ametupatia magari haya kwa ajili ya kusaidia wakuu wa wilaya waweze kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi. Tunaamini haya yataboresha sana utendaji kazi na kushughulikia changamoto za wananchi kwa wakati,” alisema Chalamila.
Akizungumzia zawadi ya gari kwa kipa Yakoub Suleiman, Chalamila alisema:
“Nilitoa ahadi wakati wa mechi ya robo fainali kati ya Tanzania na Morocco. Licha ya kufungwa bao moja, Yakoub alionyesha uwezo mkubwa na nidhamu ya hali ya juu. Hii ni kutambua mchango wake kwa taifa.”
Katika hatua nyingine, RC Chalamila alizitaka halmashauri zote za jiji la Dar es Salaam kuhakikisha zinaunda timu za michezo, hasa za mpira wa miguu, zinazomilikiwa rasmi na halmashauri husika, pamoja na kuanzisha viwanja vya michezo ikiwemo vya ngumi, ili kutoa fursa za ajira kwa vijana wenye vipaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Wakili Albert Msando, aliishukuru serikali kwa msaada wa gari hilo na kuahidi kuboresha huduma kwa wananchi.
“Kupatikana kwa gari hili kutatuwezesha kufika maeneo mengi zaidi kwa haraka na kutoa huduma bora kwa wananchi. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa msaada huu,” alisema Msando.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, aliahidi kuendeleza juhudi za kuinua michezo katika wilaya hiyo, akisema michezo ni kichocheo muhimu cha ajira na maendeleo kwa vijana.