Sakata la mwalimu aliyemuadhibu mwanafunzi Makumbusho lachukua sura mpya

Dar es Salaam. Uongozi wa Shule ya Sekondari Makumbusho iliyopo Wilaya ya Kinondoni imemuondoa kazini mwalimu Felix Msila kutokana na tukio la kutoa adhabu ya viboko kikatili kwa mwanafunzi wa kidato cha pili, Khatib Salim, huku Halmashauri ya Kinondoni ikiahidi kuchukua hatua zaidi.

Tukio hilo lilitokea Alhamisi Septemba 18, 2025 na baadaye picha mjongeo zilisambaa katika makundi mbalimbali sogozi ya WhatsApp.

Kwa mujibu wa barua ambayo Mwananchi imeiona yenye kumbukumbu namba Kumb/No/KMC/MKSS/Vol.01, Mwalimu Msila Felix ameondolewa kazi Septemba 19, 2025 na Mkuu wa Shule ya Sekondari Makumbusho, Ester Mianga.

“Kufuatia tukio ulilolifanya la kutoa adhabu kikatili kwa mwanafunzi wa kidato cha pili Khatib Salim siku ya Alhamisi Septemba 18, 2025 bila kuzingatia waraka wa elimu namba 24 wa mwaka 2002 kuhusu utoaji wa adhabu ya viboko shuleni,” imeeleza barua hiyo na kuongeza;

“Uongozi wa shule kwa kushirikiana na kamati ya wazazi umekufukuza kazi rasmi kuanzia leo Septemba 19, 2025.”

Barua hiyo ilipelekwa nakala kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Ofisa Elimu Sekondari, mwenyekiti wa bodi ya shule na mwenyekiti wa kamati ya wazazi.

Kanuni ya utoaji viboko GN namba 294 ya Julai 31, 2002 iliyozaa Waraka wa Elimu namba 24 wa 2002 kuhusu adhabu ya viboko inataka adhabu ya viboko itolewe kwa kuzingatia ukubwa wa kosa, umri, jinsi na afya ya mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja.

Lakini sheria na waraka huo vinataka adhabu itolewe na mwalimu mkuu au mwalimu mwingine atakayeteuliwa na mwalimu mkuu kwa maandishi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Septemba 22, 2025 Ofisa Elimu wa Wilaya ya Kinondoni, Mtundi Nyamuhanga  amesema tukio la mwalimu huyo linashughulikiwa kwa sasa chini ya halmashauri.

“Ninalifahamu tukio hili na linashughulikiwa, na halmashauri itatoa taarifa muda wowote kuanzia sasa,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu barua ya kufukuzwa kazi, Nyamuhanga amesema, “Hiyo barua chanzo chake ni mkuu wa shule ameandika kumwondoa mwalimu, hiyo ni mamlaka yake kwa kuwa si mwalimu wa kuajiriwa, anayejitolea anaajiriwa na mkuu wa shule na kamati ya wazazi kwa hiyo akileta chochote kinacholeta taharuki wana uwezo wa kumwondoa wao.”

Hata hivyo katika utetezi wake, Mwalimu Msila aliyehitimu katika Chuo Kikuu cha St Joseph mwaka 2024 kwa shahada ya ualimu wa masomo ya Baolijia na Kemia amesema;

“Mnamo Septemba 18, 2025 Alhamisi majira ya mchana nilitoa adhabu kwa wanafunzi kwa sababu walikuwa wanapiga kelele sana muda wa vipindi na mmoja wa wanafunzi aligomea adhabu na kuanza kubishana na mimi na kujibu majibu ya hovyo mbele ya wanafunzi wenzake.

“Nikamshika shingoni na kumpeleka ofisi ya nidhamu kwa ajili ya kutoa maelezo kwanini anabishana na mwalimu na kugomea adhabu, ni mwanafunzi wa kidato cha pili mkondo B,” alitoa maelezo yake Mwalimu huyo aliyekuwa akifundisha somo la kemia kidato cha pili.

Hata hivyo, maoni mbalimbali yaliyotolewa na watu mbalimbali mtandaoni, yalieleza kuwa kipigo hicho ni cha ukatili na hakifai kwa mwanafunzi.