TRA NA MAMLAKA ZA MAPATO EAC ZASAKA SULUHU ZA PAMOJA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA

 


Na Mwandishi wetu, Michuzi Tv 

MAMLAKA za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekutana jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kuboresha mifumo ya kodi ili kuchochea ukuaji wa biashara ndani ya Jumuiya hiyo.

Akizungumza  katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa mia moja  wa Kamati ya Kiufundi ya Mamlaka hizo leo Septemba 22, 2025 jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, alisema nchi wanachama zinapaswa kuwa na suluhu za pamoja kuondoa vikwazo vinavyokwamisha urahisi wa kufanya biashara.

 “Tunapaswa kuona namna tunavyoimarisha biashara katika ukanda wa EAC. Ni muhimu watanzania waweze kwenda Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na kwingine kufanya shughuli zao bila changamoto yeyote inayotokana na vikwazo vya kikodi. Sisi Tanzania tutaviondoa, na tunatarajia na wao pia wafanye hivyo ili kuhamasisha biashara za kikanda,” amesema Mwenda.

Amebainisha kuwa tatizo la magendo bado ni changamoto kubwa nalinachochewa na tofauti za viwango vya kodi baina ya nchi wanachama. 

Amesema Kamati hiyo itajadili mbinu za kudhibiti hali hiyo, ikiwemo kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika na kutumia teknolojia za kisasa kama akili mnemba (AI) kuwabaini na kuzuia vitendo hivyo.

Mwenda ameongeza kuwa majadiliano hayo pia yatajikita katika kukuza biashara za ndani na kupunguza kodi za ndani ili wafanyabiashara wa ukanda huo waweze kushindana ipasavyo katika masoko ya nje.

 “Tunataka kujenga taswira nzuri ya taasisi zetu kwa kuondoa rushwa na kuweka utawala unaomsaidia mlipakodi badala ya kumwonea. Ni lazima tufanye mageuzi yanayoendeshwa na teknolojia, kutumia uchambuzi wa takwimu, kuoanisha mifumo yetu na viwango vya kimataifa, na kuimarisha uwazi,” alisema.

Amesisitiza kuwa sera ya kodi itajadiliwa ili kuona namna ya kufanana kwa viwango vya ndani (tax rates), ili wafanyabiashara wanaofanya biashara katika nchi tofauti za EAC wasikumbane na changamoto kutozwa kodi kubwa au utofauti wa kodi.

 “Kwa mfano, wapo wanaozalisha bidhaa kama vigae wanapopeleka katika nchi jirani wanatozwa kodi kubwa. Tunapaswa kuondoa vikwazo hivyo na kurahisisha mifumo ya kodi iwe rahisi, inayoeleweka na ya kutabirika,” alifafanua 

Aidha, amesema wigo wa kodi bado ni finyu, hivyo kuna haja ya kurasimisha sekta isiyo rasmi, ikiwemo biashara ndogo ndogo na sekta ya dawa, ili kupanua msingi wa mapato.

Mwenyekiti wa mkutano huo, Beatus Nchota amesema wamejipanga kutoa matokeo yenye viwango vya juu vitakavyosaidia ukuaji na ustahimilivu wa uchumi wa kikanda.

 “Kadri ukanda wa Afrika Mashariki unavyokua, ni lazima mifumo yetu ya kodi ibadilike kuendana na mabadiliko ya uchumi wa bidhaa. Tunapaswa kubaki na suluhisho la pamoja, mawazo bunifu, mikakati na mbinu mpya zitakazotusogeza mbele kwa malengo ya pamoja,” amesema Nchota.

Ameeleza kuwa Kamati hiyo imelenga mikakati ya kuoanisha ubunifu na teknolojia katika ukanda huo ili kusaidia viwanda vidogo pamoja na usimamizi wa mizigo mikubwa mipakani, ikiwemo madini, gesi na shughuli za usafirishaji.

Vilevile, amesema watajadili mpango wa biashara ya kukodisha (GOS) kwa kujifunza kutoka migogoro ya zamani ya kodi na mitandao mingine ya kikanda kama ‘African Tax Administration Forum ‘(ATAF)

 “Tutathmini matumizi ya biashara yenye ufanisi katika kuboresha huduma za usimamizi wa mapato, tutatafuta mbinu za kurahisisha kodi kwenye sekta isiyo rasmi, na kufanya utafiti wa kulinganisha mifumo ya ‘Relevant Contracts Tax’ ( RCT) katika nchi wanachama ili kubaini njia bora za pamoja,” amesema.

Ameongeza kuwa watajadili pia mikakati ya mafunzo na maendeleo ya taaluma kwa lengo la kuongeza uwezo na kubakiza vipaji ndani ya mamlaka za kikanda.

Naye Mwakilishi kutoka Rwanda, Densi Mukama amesema wamejifunza kutoka Tanzania kuhusu matumizi ya risiti wakati wa manunuzi, akibainisha kuwa utaratibu huo unarahisisha utunzaji wa kumbukumbu.

“Njia hii tutaianza kwetu. Mteja anapokuwa na risiti anapata uthibitisho wa manunuzi, jambo ambalo sisi hatukuwa na utamaduni nalo,” amesema.