WAANDISHI WA HABARI WAKUMBUKISHWA KUEPUKA RUSHWA KIPINDI CHA UCHAGUZI

 Katibu Mtendaji wa THBUB, Patience Ntwina akizungumza wakati wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 22, 2025.

Picha ya Pamoja.
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewataka waandishi wa habari nchini kuepuka vitendo vya rushwa, takrima na zawadi zinazoweza kuathiri weledi na uadilifu wao wakati wa kuripoti habari za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa THBUB, Patience Ntwina, wakati wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 22, 2025 alisisitiza kuwa wanahabari ni mhimili muhimu katika kulinda demokrasia na amani ya taifa kupitia kazi zao.
“Ninyi ni muhimili wa nne unaoheshimika nchini. Msiruhusu kalamu zenu zigeuke chombo cha kupandikiza chuki au kupotosha ukweli kwa ajili ya maslahi binafsi. Epukeni rushwa na zawadi zinazoweza kuwafanya muegeme upande wa chama au mgombea fulani,” alieleza
Aidha, mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa wa kitaaluma na kimaadili kwa waandishi wa habari kuhusu haki na wajibu wao katika kipindi cha uchaguzi.
Waandishi walihimizwa kutumia mbinu za uhakiki wa taarifa (fact-checking) kabla ya kuchapisha au kutangaza habari ili kuepusha upotoshaji, lugha za uchochezi na taarifa zisizo na uthibitisho.
Ntwina, ameeleza kuwa jukumu la vyombo vya habari ni kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu sera na ajenda za kisiasa, bila upendeleo, huku vikibaki kuwa daraja kati ya wagombea, vyama vya siasa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na wananchi.
Mafunzo yanasaidia kuimarisha uhusiano kati ya vyombo vya habari na mamlaka za dola, kukuza uhuru wa habari na kuimarisha misingi ya demokrasia nchini.