MLINDA mlango wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Yakoub Suleiman Ally, amekabidhiwa gari aina ya Toyota Crown, ikiwa ni zawadi baada ya kufanya vizuri katika michuano ya CHAN 2024 iliyofanyika kuanzia Agosti 2 hadi 30 mwaka huu katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Zawadi hiyo ni ahadi aliyoitoa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakati Taifa Stars ilipokutana na Morocco katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na kukubali kuchapwa bao 1-0, ikatolewa.
Makabidhiano ya gari hilo yamefika leo Jumatatu Septemba 22, 2025 kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, huku viongozi mbalimbali wakishuhudia wakiwemo wakuu wa wilaya na wakurugenzi kutoka Halmashauri za mkoa huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Chalamila amesema katika ahadi yake alisema endapo kipa huyo hataruhusu bao atamzawadia gari aina ya Crown.
“Hata hivyo kama mnakumbuka katika mtanange ule tulifungwa goli moja lakini bwana yule alijitahidi kudaka mpaka unaona kudaka kule ni kwa sababu ya Crown.
“Yakoub alidaka vizuri mpaka wenzetu wa Simba wakamsajili, kwa kweli alionyesha kipaji cha juu na tuna imani ataenda juu zaidi baadaye.
“Lakini pia tunakukabidhi gari hii bwana Yakoub kama chachu, katika muchezo ukizingatia tuna mashindano mengine ya AFCON mwaka 2027 ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji,” amesema Chalamila.
Kwa upande wake Yakoub, ameshukuru kwa kupata gari hilo na kueleza ndio zawadi yake kubwa ya kwanza kuipata katika maisha yake.
Pia amesema zawadi hiyo inaenda kumpa chachu ya kufanya vizuri zaidi na kushukuru nchi kuwa na viongozi wanaotekeleza ahadi zao kwa vitendo kama Chalamila.
Katika michuano hiyo ambayo Taifa Stars iliishia hatua ya robo fainali, Yakoub alikaa langoni katika mechi zote tano, akiruhusu mabao mawili pekee akiwa na clean sheet tatu.
Halmashauri zatakiwa kuanzisha timu zao
Katika hatua nyingine, Chalamila ameagiza kabla mwaka huu haujaisha, kila wilaya ihakikishe inaunda timu ya mpira wa miguu itakayomilikiwa na Halmashauri.
Amesema Kinondoni tayari ina timu yake ya KMC, hivyo anataka kuona inafanyika na kwenye wilaya nyingine.
“Jiji hili ni kubwa na lina mapato makubwa yanayifika Sh300 bilioni kwa mwaka, sioni sababu kwa nini kila wilaya isiwe na timu yake, hii inawezekana.
“Tunafanya hivi kwa kuwa mchezo wa mpira ni ajira, ni biashara, ni utalii na kitambusho cha taifa letu na leo KMC haiitambulishi tu Kinondoni bali Dar es Salaam na ukisema timu za ligi kuu huwezi kuacha kuitaja,” amesema Chalamila.
Katika kulitekeleza hilo, amewataka maofisa michezo kuwasaidia wakuu wa wilaya kwenda kuanzisha timu hizo ikiwemo kwenda kwenye mashindano mbalimbali ikiwemo Ndondo Cup kusaka vipaji.
Ukiacha kwenye mpira wa miguu, kiongozi huyo pia ametaka kuanzishwa kwa kumbi zitakazotumika kwa mchezo wa ngumi kila wilaya kama ilivyofanywa Wilaya ya Kinondoni ambapo mara nyingi kampuni ya Mafia imekuwa ikiutumia kwenye mashindano ya ngumi.