AKU yaikosha Lindi mafunzo ya ualimu

Dar es Salaam. Uongozi wa Mkoa wa Lindi umesema mradi wa kuwafundisha wakufunzi umesaidia kuwajengea uwezo watendaji kuanzia ngazi elimu, kata, shule hadi halmashauri za mkoa huo.

Mradi huo unaoitwa ‘Foundations for Learning’ ulikuwa unatekelezwa na Taasisi ya Maendeleo ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, Afrika Mashariki (IED, EA) kuanzia mwaka 2022 hadi 2025 katika Chuo cha ualimu Nachingwea.

Pia, mradi huo ulihusisha kuwajengea uwezo wakufunzi waliotoka wilaya za Ruangwa, Mtama, Manispaa ya Lindi, na Nachingwea, kwa muda wa miaka mitatu wakifundishwa programu maalumu na mahususi inayolenga kuwapa stadi muhimu kuwa walimu wa karne ya 21.

Wakufunzi hao walifundishwa moduli nane zilizojikita katika mbinu za kisasa za ufundishaji, kujenga mazingira ya ujifunzaji yenye usawa wa kijinsia na matumizi ya teknolojia katika elimu kupitia ujumuishaji wa Tehama.


Taarifa kwa vyombo habari iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) leo Jumanne Septemba 23, 2025 imeeleza Ofisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Lindi, kulwa James ameeleza hayo katika mahafali yaliyofanyika jana Nachingwea mkoani Lindi.

Amesema mradi huo umekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya elimu mkoani humo, hivyo uongozi wa Lindi unaahidi kuwa elimu waliyoipata wataalamu hao haitapita hivihivi, badala yake wataandaa programu maalumu ili kufikisha kwa walimu wasiopata fursa hiyo.

“Mwaka jana baadhi yenu tuliwatumia kwa kuwapitisha kwenye baadhi ya halmashauri na kuwafundisha walimu walioko huko, lakini mwaka huu pia ifanyike hivyo hivyo. Tutatengeneza mpango maalumu wa kuwagawa katika halmashauri zetu,” amesema James.


James amewapongeza walimu walioamua kujiendeleza kielimu kupitia mradi huo, akisema si jambo jepesi mtu kuingia tena darasani lakini wao waliamua kusoma ili kujiongezea maarifa zaidi.

“Nyie mliona umuhimu wa kupikwa upya, kusoma kuna maana yake mmekwenda kurudia ili kujiimarisha zaidi. Baada ya kupita kwenye chekecheke la miaka minne sasa hivi mmekuwa wapya,”

“Jisikieni ni watu wapya sasa kama ambavyo mlivyomaliza shahada yenu ya kwanza au shahada za uzamili, mkiwa na uzoefu wa kutosha. Mmejifunza mambo mengine ikiwemo kuandaa mazingira ya shuleni,” ameeleza.

Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Elimu, Afrika Mashariki (IED,EA) ya Aga Khan, Profesa Jane Rarieya, amesema jumla ya walimu 29 walishirikia katika mafunzo hao kwa miaka minne wakijifunza namna ya kuwa viongozi na waelimishaji kwa walimu watarajiwa kupitia uongozi na uelekezi.

“Vilevile, walishiriki katika uanzishaji wa ‘Makerspace’ eneo la kukuza ubunifu na matumizi ya rasilimali zilizopo. Mmeimarisha ujuzi wenu wa kuwaongoza walimu wanafunzi wakati wa mazoezi yao ya ufundishaji,” amesema Profesa Rarieya.

Meneja wa mradi huo, Dk Nyagwegwe Wango amesema kumekuwa na mafanikio makubwa, huku akikipongeza Chuo cha Ualimu Nachingwea mkoani Lindi ambacho kimekuwa msingi mzuri wa kuandaa walimu.

“Nachingwea imeandaa walimu wazuri wanaokwenda kushirikiana na wakuu wa shule nyingine. Nimepata bahati ya kuzunguka katika shule mbalimbali, nimejionea mafanikio makubwa yaliyopatikana,”

“Tumeona uwekezaji mkubwa uliofanya na Aga Khan ulivyozaa matunda, tunajivunia baada ya kufanyika katika mkoa wa Lindi,”amesema Dk Wango.