Njombe. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimewaahidi wananchi wa Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe ujenzi wa visima vikubwa 150 vitakavyowawezesha kulima kilimo cha umwagiliaji huku vitongozi zaidi ya 200 visivyo na umeme vitaunganishiwa huduma hiyo.
Pia, ujenzi wa shule mpya za msingi tatu, barabara kwa kiwango cha lami na changarawe na kuboresha huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya na Zahanati na ujenzi wa maegesho matatu makubwa ya magari.
Ahadi hizo, zimetolewa leo Jumanne, Septemba 23, 2025 na mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi katika mkutano wa kampeni uliofanyikia Stendi ya mabasi ya Igwachanya, Jimbo la Wanging’ombe.
Dk Nchimbi amesema, ahadi hizo na nyingine zitatelekezwa iwapo tu wananchi wa Wanging’ombe watajitokeza kwa wingi Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kukipigia kura chama hicho ili kiendelee kusalia madarakani.
Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amemwombea kura mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan ambaye kwa sasa yupo mkoani Mtwara naye akizisaka kura. Pia, Dk Nchimbi amemwombea kura Dk Festo Dugange kuwa mbunge na madiwani.
Eneo la kilimo lilianza kuelezwa na mgombea ubunge, Dk Dugange kwamba wananchi wa Wanging’ombe wanajishughulisha zaidi na kilimo hivyo wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la kipekee na Dk Nchimbi akasema:”Tutachimba visima 150 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Pia, mabwawa makubwa yatajengwa.”
Dk Nchimbi amesema kama Rais Samia alivyoahidi, mbolea na mbegu za ruzuku zitaongezwa na zitatolewa kwa wakati na watakaosababisha kuchelewa watachukuliwa hatua.
“Oktoba 29 mkituchagua, tunakwenda kuiboresha zaidi Hospitali ya Wilaya, iwe na vifaa vya kisasa, tutasogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kujenga vituo vipya vitatu vya afya na Zahanati mpya tano,” amesema Dk Nchimbi.
Amesema, kilio cha mgombea ubunge cha baadhi ya vitongoji havina umeme, Dk Nchimbi amesema katika awamu ya pili utatekelezwa katika vijiji na vitongoji vyote:”Tumedhamiria miaka mitano ijayo, kitongoji hata kimoja kisiwepo Wanging’ombe ambacho hakina umeme.”
Amesema, habari ya barabara kama alivyoeleza Dk Dugange nayo haikuachwa nyuma zitajengwa kwa kiwango cha lami na changarawe ili kurahisisha shughuli za usafirishaji.
Ahadi ya elimu haikuwa nyuma, Dk Nchimbi ameahidi ujenzi wa shule mpya tatu, kuongeze madarasa mapya 60 na ujenzi wa maabara mpya 10 za sayansi.
“Idadi ya watoto wanaongezeka, tutaongeza madarasa mapya 75 katika sekondari zetu, nyumba mpya za walimu 20 na ili watoto wakae shule basi tutajenga hosteli 20,” amesema huku akishangiliwa.
Msongamano wa magari wilayani humo, Dk Nchimbi ameahidi ujenzi wa maegesho ya magari makubwa matatu na vituo vipya vya magari vitatu pamoja na ujenzi wa viwanda vinavyoendana na mahitaji ya eneo hilo.
Awali, Mgombea Ubunge wa Wanging’ombe, Dk Festo Dugange amebainisha kile kilichofanyika jimboni humo tangu Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi 19, 2021.
Samia akiwa Makamu wa Rais aliapishwa siku hiyo kuwa Rais wa Tanzania, kuchukua nafasi ya John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Dk Dugange amesema haijawahi kutokea katika historia ya jimbo hilo kupata fedha nyingi za miradi mbalimbali ya maendeleo kama kipindi cha utawala wa Rais Samia.
“Katika sekta ya afya, mwaka 2021 wakati Rais Samia anaingia madarakani, hatukuwa na Hospitali ya wilaya, kulikuwa na upungufu mkubwa wa watumishi, lakini
Sh18 bilioni tulipokea na tumejenga Hospitali ya wilaya, vituo vipya vya afya 13 na Zahanati mpya 20 zimejengwa,” amesema Dk Dugange.
Amesema katika kata 21, kata 14 zina vituo vya afya, magari ya wagonjwa yamepelekwa wilayani humo na vifaa tiba na watumishi maeneo mbalimbali ya Wanging’ombe.
Dk Dugange ambaye pia ni Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) amesema, jitihaza hizo kwenye sekta ya afya, imesaidia kupunguza vifo vya wajawazito akitolea mfano, kulikuwa na vifo 563 katika vizazi hai 100,000 lakini kwa sasa vimepungua hadi vifo 104 katika vizazi hai 100,000.
Kuhusu elimu, Dk Dugange amesema kata nne hazikuwa na shule za sekondari, lakini ndani ya kipindi cha Rais Samia, walipokea Sh18.4 bilioni ambazo zimefanikisha kujenga shule za msingi 13 na za sekondari 11 pamoja na madarasa zaidi ya 400 yakijengwa.
“Wanging’ombe ni moja ya wilaya iliyopata bahati ya kijengewa Shule ya Wasichana ya sayansu kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita ambapo Sh5 bilioni zilitumika,” amesema.
Eneo la barabara, mgombea ubunge huyo anayetetea nafasi hiyo kwa miaka mitano mingine amesema, kulikuwa:”Na changamoto kubwa sana ya barabara, wakulima wa parachichi, mbao, viazi mviringo, magari yalikuwa yanakwama na kusababisha hasara kubwa.”
Amesema kuanzia mwaka 2021, walipokea Sh32.5 bilioni ambazo ziliwezesha kujengwa zaidi ya Kilomita 535 kwa kiwango cha lami, changarawe na udongo na kupunguza adha kwa wananchi na wafanyabiashara.
Dk Dugange amemwomba Dk Nchimbi baada ya uchaguzi kumaliza na kuundwa Serikali, kutupia jicho la kipekee maeneo ambayo barabara bado ili kuifungua zaidi Wanging’ombe.
Katika huduma ya maji, Dk Dugange amesema Sh77.7 bilioni wamezipokea kuanzia mwaka 2021 ambapo miradi mbalimbali inatekelezwa na ikikamilika ikiwemo mradi wa miji 28 hali itabadilika.
“Kwa sababu hali ya maji ni ngumu, tunaomba tuendelee kupewa fedha ili wananchi wapate maji na kuondokoana na changamoto hii. Tunaimani na Serikali yetu, tunaamini mradi huu wa miji 28 utakamilika na kuondoka kabisa shida ya maji kwa wananchi wa Wanging’ombe,” ameomba Dk Dugange.
Mwaka 2021 wakati Samia anaapishwa, Dk Dugange amesema ni vijiji 48 tu kati ya 108 vilivyokuwa na umeme huku vitongoji 528 havikuwa na huduma hiyo lakini kwa sasa vijiji vyote na vitongoji 207 vina umeme.
Ameomba vitongoji vilivyobaki viunganishwe na Dk Nchimbi amesema miaka mitano ijayo wakishinda vitongoji vyote vilivyobakia vitaunganishiwa huduma hiyo.
Aidha, Dk Dugange amewasiliasha ombi la kujengwa kituo cha umeme wilayani humo ili kuondoa adha ya wenye viwanda kukosa huduma hiyo kwani amedia wanapokea umeme kwa njia moja kutoka Makambako hali inaoufanya kuwa na nguvu kidogo.
“Jimbo letu ni la wakulima, linahitaji viwanda vya kuchakatwa mazao yetu lakini tuna laini moja kutoka Makambako, tunaomba ijenga ‘sub station’ ili wananchi wenye viwanda wasikose umeme,” amesema Dk Dugange.
Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Njombe, Deo Sanga maarufu Jah People amesema makapu ambayo wanawake wanabeba wana maanisha kura zitajaa mule.
Jah People amesema mkoa wa Njombe huwa unaongoza kitaifa kwa kura na sasa wilaya zinashindana hivyo amewaomba wananchi Oktoba 29, 2025 kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Katika hilo, Dk Nchimbi amesema:”Nimekuwa naona vikapu sijui maana yake, kumbe maana yake mtajaza kura za Samia, wabunge na madiwani, basi mmenifurahisha sana.”
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu na mratibu wa kampeni hizo kanda ya nyanda za juu, Salum Asas amesema tangu kampeni za uchaguzi zilizoanza Agosti 28, 2025 hadi sasa, hakuna matusi au vijembe bali wanajielekeza kueleza nini wamekifanya na watakifanya miaka mitano ijayo.
“Watu hawali matusi, watu hawalimi matusi. Watu wanataka maendeleo na watafanyiwa nini, chama kinasisitiza amani na upendo. Kwa hiyo tunakipongeza sana chama chetu kwa kuhakikisha kinaendelea kueleza kile kitakachowanyja wananchi.”
Endelea kufuatilia Mwananchi