Iringa. Katika hatua inayoonyesha mshikamano wa kijamii na kisiasa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeamua kugharamia masomo ya watoto wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Iringa Mjini, marehemu Frank Nyalusi.
Akizungumza leo Jumatatu, Septemba 22, 2025, katika ofisi za chama hicho zilizopo Veta Manispaa ya Iringa, Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami amesema chama kimeanza kugharamia ada na mahitaji ya shule ya watoto wa marehemu zilizofikia zaidi ya Sh2 milioni.
Familia ya marehemu imeeleza hatua hiyo kuwa ni faraja kubwa baada ya kumpoteza mpendwa wao aliyehudumu kwa uadilifu na kujitoa kwa wananchi.
Mdogo wa marehemu, Maltino Kindole amesema msaada huo ni ishara ya upendo na mshikamano unaoendelea kuwafariji katika kipindi kigumu cha maombolezo.
Amefafanua kuwa watoto wanne wa marehemu ndio walengwa wa msaada huo akiwataja kuwa ni Gloria Nyalusi, mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Pandahill jijini Mbeya, Bryan Nyalusi anayesoma darasa la tano, Donald Nyalusi darasa la tatu, wote katika Shule ya Msingi Luindo mkoani Iringa na Anna Nyalusi aliyemaliza darasa la saba mwaka huu katika Shule ya Sunflower, Iringa.
Kwa upande wake, Wakili Emmanuel Chengula ambaye amekuwa karibu na familia hiyo, amesema safari ya elimu ya watoto hao bado ni ndefu na inahitaji mshikamano wa jamii nzima. Amebainisha kuwa kundi la michango lililoanzishwa wakati marehemu akiwa mgonjwa sasa limeelekezwa kusaidia malezi na masomo ya watoto hao.
“Kuna kundi tulilokuwa tunachangia wakati Nyalusi anaumwa, lakini sasa litatumika kusaidia watoto wake. Safari bado ni ndefu, wanahitaji kuungwa mkono hadi pale watakapohitimu masomo,” amesema Chengula.
Michael Kyando, Katibu wa Chadema Jimbo la Iringa Mjini amesema chama kimefarijika kuona wananchi na wadau mbalimbali wakiendelea kujitolea kusaidia familia hiyo na kwa niaba ya kamati tendaji ya jimbo, aliwashukuru wote walioweka mchango kuanzia kipindi cha kuugua kwa Nyalusi hadi mazishi yake.
Aidha, Kyando amebainisha kuwa chama kipo kwenye maandalizi ya kutangaza uchaguzi mpya wa Mwenyekiti wa Jimbo la Iringa Mjini ili kuendeleza kazi na dira iliyokuwa imewekwa na marehemu.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema Kanda ya Nyasa, Charles Ndenga amesema chama kinaendelea kuwa kitu kimoja licha ya pengo lililoachwa na Nyalusi, huku akisisitiza kuwa uamuzi wa chama kugharamia masomo ya watoto wake ni ishara ya uongozi wa huruma na mshikamano wa kweli.
Viongozi wa vijana pia hawakubaki nyuma, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema Mkoa wa Iringa, Ibrahimu Myovela amewatoa hofu wananchi waliokuwa wakieleza mashaka juu ya ushiriki wa viongozi wa juu, akisema Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai, alishiriki kikamilifu katika kipindi cha ugonjwa na msiba wa Nyalusi.