Dar es Salaam. Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) kimetoa wito kwa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuzingatia maadili ya taaluma ya sheria na misingi ya ueledi katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wanachama wake.
Hii ni kufuatia tamko la TLS linalowataka wanachama wake kusitisha kushiriki katika utoaji wa msaada wa kisheria, kama njia ya kushinikiza hatua zichukuliwe dhidi ya vitendo vya udhalilishaji alivyodaiwa kufanyiwa mwanachama wake, Deogratius Mahinyila, alipokuwa mahakamani.
PBA imesisitiza kuwa, ingawa ni haki kwa chama chochote cha kitaaluma kulinda maslahi ya wanachama wake, hatua zinazochukuliwa zinapaswa kuendana na miongozo ya kitaaluma na kuhakikisha kuwa hazileti athari kwa wananchi wanaotegemea huduma za kisheria.
Hata hivyo, Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi amejibu akisema tayari Serikali inafanyia kazi madai yao na kilichofanywa na PBA, kusemea mambo yanayofanyiwa kazi, ni utovu wa nidhamu kwenye tasnia hiyo.
Ikumbukwe, Septemba 18, 2025, TLS ilielekeza wanachama wake kusitisha ushiriki wao kwenye kesi za msaada wa kisheria za jinai ikiwa ni sehemu ya kulaani shambulio dhidi ya mwanachama wake, Deogratius Mahinyila.
Msimamo mwingine wa TLS ulikuwa ni kufanyika maandamano Septemba 22, nchi nzima, kulaani tukio la kushambuliwa na kudhalilishwa kwa wakili Mahinyila na askari wa Jeshi la Polisi, lililotokea Septemba 15, 2025 katika viwanja vya Mahakama Kuu, Masijala ndogo ya Dar es Salaam.
Taarifa hiyo ya TLS ni msimamo wa baraza lake la uongozi uliotolewa rasmi Septemba 18, 2025 na kusainiwa na Rais wa chama hicho, Boniface Mwabukusi.
Hata hivyo maandamano hayo hayakufanyika kutokana na mazungumzo yanayoendelea baina ya upande wa Serikali na TLS.
Kauli ya mawakili wa Serikali
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Septemba 23, 2025, Mwenyekiti wa PBA, Ado Novemba amesema TLS ni chama cha kitaaluma, hivyo ni vyema maamuzi wanayotoa yaongozwe na weledi, ubora na utii wa sheria na si misukumo ya unaharakati.
“Kuna taaluma na mtu kuwa mwanaharakati. Tumeona hayo yanatokea na bora tuseme, wajibu wa wakili ni kulinda heshima ya mahakama na kuhakikisha kwamba shughuli zake zinabaki ndani ya mipaka ya kitaaluma,” amesema.
Novemba amesema TLS inapaswa kuzingatia weledi, ubora, heshima na kudumisha taaluma ya uwakili kwa mujibu wa sheria.
“Wakili hana mamlaka kutumia taaluma yake kama jukwaa la siasa au vitendo visivyoheshimu sheria. Kwa msingi huo, maamuzi waliyotoa TLS yanalenga kuzuia mawakili wasitoe msaada wa kisheria, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu na wajibu wa taaluma hiyo,” amesema.
Novemba amesema jukumu la kwanza la wakili ni kutoa msaada wa kisheria na haki lazima ionekane inatendeka kwa wenye uwezo na wasio na uwezo.
Takwa hilo amesema, siyo uamuzi wa mawakili pekee, bali msaada wa kisheria ni takwa la kisheria.
“Huduma hizi zimekusudiwa kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini, ambao ndio wengi, wapate msaada, wahudumiwe na wasipoteze haki zao. Wao wanakuja kutoa azimio la kuwataka mawakili waache kutoa msaada wa huduma za kisheria wakati ni takwa la kisheria,” amesema.
Mwabukusi katika majibu yake amesema; “Serikali ina msemaji wake, na mtu asiye kuwa msemaji kusemea mambo ambayo tayari yanafanyiwa kazi na mamlaka ya juu katika tasnia ni utovu mkubwa wa nidhamu,” amesema.
Amesema mawakili wa Serikali hawana mamlaka ya kuzungumzia majukumu na maamuzi ya mawakili wa kujitegemea.
“Mambo ya kanisani muachie mchungaji na yale ya msikitini muachie imamu. Vivyo hivyo, majukumu ya TLS na wanachama wake wa kujitegemea yako chini ya TLS na si hao wanasheria.”
Mawakili wa kujitegemea wanachopinga si kazi yenyewe ya msaada wa kisheria, bali mazingira hatarishi ya kazi, vitisho na manyanyaso ambayo yamekuwa yakifanywa dhidi ya mawakili na wananchi ndani ya maeneo ya mahakama na katika utekelezaji wa majukumu yao yanayofanywa na Jeshi la Polisi,” amesema.
Mwabukusi amesema bado hakuna uamuzi wa mgomo au maandamano na wapo kwenye mazungumzo, na hao mawakili wa Serikali hawajalizungumzia.
Amesema ni upotoshaji kuzungumzia maadili ya uwakili bila kwanza kuhakikisha usalama wa wakili na mazingira bora ya kazi.
Rais huyo wa TLS amesema chama hicho ndicho chombo pekee kinachowakilisha maslahi ya mawakili wa kujitegemea na kina wajibu wa kulinda heshima, hadhi na uhuru wao wa kitaaluma.
“Kama kuna wakili wa Serikali anadhani maamuzi haya si sahihi, basi suluhisho si kutoa kauli za kisiasa, bali ni kujiunga na sekta binafsi na kushiriki kwenye maamuzi ya TLS kama mwanachama wa kujitegemea,” amesema.