DC Nyamwese aanika fursa za uwekezaji Handeni

Na Augusta Njoji, Handeni TC

MKUU wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, ametoa rai kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwamo viwanda vya kuchakata machungwa, ili kuchochea maendeleo ya wilaya hiyo.

Akifungua kikao cha Baraza la Biashara la Wilaya kilichofanyika mjini Handeni Septemba 23, 2025, Nyamwese ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, amezitaka Halmashauri za Wilaya na Mji wa Handeni kupitia Maofisa Mipango kuandaa vitini vinavyoainisha maeneo ya uwekezaji, ili kurahisisha wawekezaji kubaini fursa zilizopo.

Amesema serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya Handeni na kupanua wigo wa ajira kwa vijana, kutokana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kuonesha wilaya hiyo ina wakazi zaidi ya 400,000, ambapo asilimia 65 hadi 70 ni vijana.

“Wilaya yetu inakua kwa kasi, hivyo ukuaji huu ni fursa kwenu wafanyabiashara na wawekezaji. Nitoe wito kwenu kuwa wabunifu ili kuchochea maendeleo ya wilaya yetu. Hapa Handeni tuna fursa ya madini, tufungue milango ya uwekezaji,” amesema Nyamwese.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Nyamwese amesisitiza kuendeleza mazao ya kimkakati ikiwamo mkonge, pamoja na uwekezaji kwenye viwanda vya machungwa kutokana na wilaya hiyo kuzalisha kwa wingi.

Aidha, katika sekta ya utalii, Mkuu huyo ametaka kuandaliwa mkakati wa kitaalamu wa kutunza vivutio vya utalii na vya kihistoria, ikiwamo eneo walilopotea kungwi na mwali, pamoja na nyumba aliyolala Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuandaa makala maalum kuhusu maeneo ya kihistoria kwa kushirikisha wazee wa maeneo husika kutoa shuhuda zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Wilaya hiyo, Adolf Lyakundi amebainisha kuwa ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi ndio msingi wa kuchochea maendeleo ya Handeni.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju, amesema halmashauri hiyo imejipanga kuandaa Mpango kabambe wa Mji huo (Master Plan) kwa ajili ya kupanga na kupima ardhi ili kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji.

Wafanyabiashara waliokuwepo wameshukuru serikali kwa kuendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili, wakisema hatua hiyo inawaongezea imani katika kuwekeza na kukuza biashara zao.