MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wakulima wa mbaazi na ufuta katika wilayani Tunduru mkoani Ruvuma kwamba Serikali inaendelea na mazungumzo na Serikali ya India kwa ajili ya kuuza mazao hayo.
Akihutubia wananchi wa Kijiji cha Nakapanya wilayani Tunduru mkoani Ruvuma leo Septemba 23,2025 ,Dk.Samia ambaye anaendelea na mikutano kuomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29,2025 amesema kuna miaka bei za mazao zinapanda na kipindi kingine zinashuka.
Amesema sasa hivi mbaazi na ufuta zinazalishwa katika kipindi ambacho nchi nyingi duniani zimezalisha zao hilo.”Kwa maana hiyo bei iliyopo duniani hasa kwa wenzetu India ambao tunawauzia, wamezalisha kwa wingi kipindi hiki kwa hiyo wametushushia bei.
“Hata hivyo tupo nao kwenye mazungumzo, tunazungumza nao bei isishuke zaidi ya asilimia 60 ya bei ya mwaka jana. Tunazungumza nao, niwatie moyo kwamba bado serikali yenu
Pamoja na kuzungumzia bei ya mazao hayo amesema pia serikali inasambaza mbolea za ruzuku na pembejeo za kilimo.
Aidha Serikali imeendelea na kazi ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji ambazo zitawezesha wakulima kusalisha mazao mara mbili kwa mwaka.
“Natambua Nakapanya ni wazalishaji wazuri wa mazao ya kilimo. Tupo na nyinyi kwa ruzuku ya pembejeo na mbolea.
“Najua tumeanza kujenga mabwawa ambayo bado hayajakamilika nayo tutakuja kuyakamilisha kwani yapo katika hatua mbalimbali,” amesema Dk.Samia.
Kwa upande wa wanyama waharibifu, amesema anatambua changamoto hiyo ya wanyamapori wanaovamia mashamba.
“Natambua hapa kuna kituo kimoja tumejenga na kituo cha pili tunakijenga pale Lukumbile lakini najua kuna askari katika maeneo matano mengine zote hizo ni jitihada za kuwafukuza wanyama hao wasiharibu mashamba na wasiumize watu
“Jana nikiwa pale Tunduru serikali tumenunua ndege tano zisizokuwa na rubani za kufukuza wanyama. Zinafanyakazi maeneo mbalimbali kama tatizo likizidi zitaletwa ndege zingine,” amesema.
Kuhusu maendeleo kwa wananchi wa Nakapanya wilayani Tunduru amesema anatambua maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika eneo hilo lakini pia hata hivyo bado kuna baadhi ya changamoto zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi.
“Serikali inaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.Hapa Nakapanya bado kuna mahitaji mengi nikiangalia nauona umeme na najua umefika vijiji vyote sasa tunaunganisha kwenye vitongoji.
“Lakini kuna suala la afya. Najua tumejenga vituo vya afya, zahanati na ninakumbuka vyema Kijiji cha Namiungo ilikuwa tujenge kituo cha afya lakini hatukufanikiwa,” alieleza.
Dk. Samia alitoa ahadi kwa wananchi kujenga kituo hicho cha afya ili wananchi wapate huduma kwa karibu.
Vilevile, amesema kuna maboma ya zahanati ambayo ujenzi wake haujakamilika, hivyo serikali inakuja kuyamalizia.
Kuhusu suala la maji, ameeleza kuwa bado kuna baadhi ya maeneo yanakabiliwa na uhaba wa maji licha ya serikali kujitahidi kufikisha huduma hiyo.”Lengo la serikali kama ilivyoahidi kupitia ilani ya uchaguzi ni kila mwananchi apate maji safi na salama.
“Kazi inayoendelea ni kwenda kuheshimu na kuupa hadhi utu wa mtu na ndiyo maana tunasema Kazi na Utu, tunasonga mbele.