BAADA ya kuitumikia Tanzania Prisons kwa miaka 16, aliyekuwa nahodha wa timu hiyo Jumanne Elfadhil ametangaza kupumzika akiahidi kuisaidia timu hiyo kwa mawazo atakapohitajika, huku akitoa neno juu ya matokeo ya mechi mbili kwa Wajelajela hao.
Elfadhil amekuwa katika kikosi hicho tangu alipoanza kuitumikia mwaka 2009 alipojiunga nayo, kwa sasa amesema hatarajii kurejea uwanjani tena na badala yake msaada wake utabaki nje ya uwanja.
Prisons haijaanza vyema msimu huu wa 2025/26 baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo, ikianza kwa kipigo cha 1-0 kutoka kwa Coastal Union sawa na kile ilichokutana nacho juzi kwa Namungo zote zikiwa mechi za ugenini na kuiacha iburuze mkia wa msimamo wa ligi yenye timu 16.
Akizungumza na Mwanaspoti, Elfadhil ambaye anasifika kwa nidhamu ndani na nje ya uwanja, alisema kwa sasa ameamua kupumzika kutokana na majeraha yanayomuandama, lakini hatarajii kurejea tena uwanjani.
Kiungo huyo alisema iwapo atahitajika kwa namna yoyote, msaada wake utabaki katika kushauri lakini siyo kucheza uwanjani, akieleza kuwa alichofanya kwa muda wote kitoshe na kuwapisha wengine kuonyesha uwezo na vipaji.
“Nimepumzika kwa muda usiojulikana, si tu kuwa majeruhi lakini niwapishe wengine waendeleze tulipoishia, ikitokea wakanihitaji kwa msaada wowote nitakuwa tayari kushauri ila siyo kucheza uwanjani,” alisema Elfadhil.
Aliongeza matokeo ya kupoteza mechi mbili mfululizo hayawezi kutafsiriwa kama ni timu kufanya vibaya, ila ni ugumu tu wa kawaida.