NDANI ya siku sita kutoka leo, wakati wowote Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linaweza kuingia kwenye hatua kubwa ya mabadiliko kwa kuteuliwa katibu mkuu mpya.
Taarifa kutoka TFF ni, Katibu Mkuu wa sasa wa shirikisho hilo, Wilfred Kidao yuko kwenye hatua za kuachia nafasi hiyo.
Inaelezwa, Kidao ameshaandika barua ya kuomba kutoendelea na majukumu hayo, ikiwa ni kumpa nafasi Rais wa TFF, Wallace Karia, kufanya uamuzi wa kuteua mtendaji mpya.
“Kidao ameshawasilisha maombi kwamba hataendelea kuwa kwenye nafasi hiyo, amewasilisha kwa Rais (Karia) moja kwa moja, ambaye kimsingi ndiye aliyemteua wakati anaingia madarakani kwa mara ya kwanza kwenye utawala wake,” alisema mmoja wa mabosi wa juu wa TFF.
“Unajua kwa kuwa ameomba yeye, nadhani ameamua kumpa nafasi rais mapema kuteua au kuanza kufikiria mrithi wake, nadhani wakati wowote mtatangaziwa.”
Wakati taarifa zikisema hivyo, imefahamika kwamba licha ya Kidao kutangulia kuandika barua hiyo, inaelezwa mkataba wa mtendaji huyo, ulikuwa unafikia tamati Septemba 30, 2025.
Kidao amedumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka minane tangu alipoteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 akiwa amekaa kwenye kiti hicho kwa mihula mitatu tofauti ya uongozi wa Karia ndani ya shirikisho hilo.