Kazi imeanza… Simba yamtolea macho Gamondi

BAADA ya Simba kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Gaborone United ugenini Botswana katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wikiendi iliyopita, mjadala ni kocha Fadlu Davids aliyeikacha timu hiyo na kutajwa kuibukia Raja Casablanca ya Morocco.

Raja ndio klabu ya mwisho kwa Msauzi huyo kuitumikia kabla ya kutua Simba msimu uliopita ambao aliwafikisha Wekundu wa Msimbazi katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Baada ya Fadlu kutimka kuna jipya limeibuka. Mwanaspoti limezipata za ndani kuwa uongozi wa Simba licha ya kutotoa ufafanuzi hadi jana kuhusu kuondoka kwa kocha huyo, uongozi wa Wanamsimbazi, unaendelea na mchakato kimya kimya kusaka mbadala na tayari umepiga hodi Singida Black Stars kuulizia uwezekano wa kumpata Miguel Gamondi.

Mwanaspoti linajua kwamba kuna kitu kinaendelea kati ya Gamondi na Simba na tayari wamewasiliana kuona namna ya kumpata Muargentina huyo ingawa inafahamika kuwa bado ana mkataba wa kuinoa Singida BS inayoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikianza na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.

Chanzo cha uhakika kutoka kwa rafiki wa karibu wa Gamondi kimelihakikishia Mwanaspoti kuwa ni kweli Simba imeonyesha nia ya kumhitaji kocha huyo na kufanya naye mazungumzo na ameiagiza kwenda kwa viongozi kwani ndio kwanza anautumikia mkataba aliosaini mwanzoni mwa msimu huu.

“Ni kweli Simba wamemtafuta Gamondi ambaye majibu yake ni kwamba bado ana mkataba na Singida Black Stars na kuwataka wazungumze na viongozi wa timu hiyo kama kutakuwa na uwezekano wowote wa kuweza kumpata,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;

“Kwa upande wa Gamondi na Simba kwa sasa hakuna kinachoendelea zaidi kwani amewapa mwanya wa kuzungumza na uongozi wa timu hivyo hao ndio watu sahihi wa kutoa taarifa kama kocha ataendelea kubaki au anaenda Simba.”

Gamondi tangu amejiunga na Singida BS, tayari ameiongoza timu hiyo kutwaa taji la Kagame Cup na ameisaidia timu hiyo kuanza vizuri kimataifa akianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda na leo ataisimamia timu hiyo ikicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya KMC.

Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia Nasreddine Nabi, ambaye aliipa mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Tangu alipoteuliwa Yanga, Gamondi aliiongoza timu hiyo kucheza jumla ya mechi 40 za Ligi Kuu Bara zikiwamo 30 za msimu wa 2023-2024 na 10 za msimu wa 2024-2025, ambapo kiujumla kati ya hizo alishinda 34, sare nne na kupoteza pia nne.

Katika mechi hizo 40, safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho cha Gamondi ilifunga jumla ya mabao 85 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18, ambapo kiujumla kwa misimu miwili alikusanya pointi 104.

Gamondi alishinda mataji matatu na Yanga akianza na Ligi Kuu msimu wa kwanza na kukifanya kikosi hicho kufikisha jumla ya mataji 30 tangu mwaka 1965 ligi hiyo ilipoanzishwa, pia akachukua Kombe la Shirikisho (FA) na Ngao ya Jamii.

Gamondi aliipeleka timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25, kufuatia kufanya hivyo mara ya mwisho 1998.

Ushindi wa mabao 4-0 ilioupata Yanga dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria Februari 24, 2024, katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, ulimfanya Gamondi kuandika rekodi mpya ya kuivusha robo fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia yao. Aliivusha tena hatua ya makundi kwa mara ya pili mfululizo, lakini akatimuliwa na nafasi yake ilichukuliwa na Sead Ramovic aliyeshindwa kuipeleka robo fainali kwa kuvuna pointi nane katika kundi lake, ikitanguliwa na Al Hilal ya Sudan iliyoongoza na MC Alger iliyokuwa ya pili kwa kupata pointi tisa.