Soma simulizi hii: “Jina langu ni Amina, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya umma iliyo mkoani Pwani.
Kila Jumatatu asubuhi tunakuwa na kipindi cha Kemia, kipindi ambacho kwa wengi wetu kingepaswa kuwa cha kusisimua, majaribio, mabadiliko ya rangi ya kemikali, na mvuke unaopanda juu ya mitungi ya maabara.
Lakini kwetu sisi, yote hayo yamesalia kuwa hadithi tu kwenye vitabu. Mwalimu wetu huandika michoro ya maabara ubaoni, akiigiza jinsi acid inavyo ‘react: na alkali, huku sisi tukitazama kwa macho ya hamu na ndoto zisizo na uhakika.
Nakumbuka mara ya kwanza kusikia kuhusu sulfuric acid nilivutiwa sana. Nilijiuliza: Je, ina rangi gani? Inanuka kama nini? Inayeyusha chuma kweli? Lakini maswali hayo yalibaki ndani ya kichwa changu, yakiwa hayajapata majibu ya moja kwa moja kwa sababu hata chupa ya kemikali hiyo hatujawahi kuiona.
Mara moja tulipelekwa kwenye maabara ya shule jirani kwa ziara ya kielimu, lakini hata huko, vifaa vilikuwa vichache, na wanafunzi tulizuiwa kugusa chochote, tukabaki watazamaji wa maajabu ya kisayansi yaliyokuwa mbali na uhalisia wetu.
Hali hii imefanya somo hili na mengineyo ya sayansi kuwa magumu na ndoto kwa wengi wetu. Tunajifunza vitu kwa nadharia pekee, bila nafasi ya kushiriki kwa vitendo, jambo linalotufanya tuwe kama watu wanaofundishwa kuogelea bila kuingia majini.
Simulizi ya Amina inaakisi uhalisia wa masomo ya sayansi katika shule nyingi nchini. Ukosefu wa maabara na vifaa unawakosesha Wanafunzi haki ya kujifunza masomo hayo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Takwimu za elimumsingi (BEST, 2023) zinaonesha kuwa ni takribani asilimia 60 pekee ya shule za sekondari zenye maabara, na chini ya nusu ya hizo ndizo zilizo na vifaa vya kutosha kwa ajili ya mafunzo ya vitendo.
Hali mbaya zaidi katika shule za umma zenye idadi kubwa ya wanafunzi lakini zikiwa na rasilimali chache. Walimu wengi hujikuta wakibuni njia mbadala za kufundishia kwa kutumia vifaa vya kawaida ili kuiga majaribio ambayo kimsingi yanahitaji vifaa na kemikali halisi.
Hali hii inasababisha ndoto ya Tanzania ya kuinua ubora wa elimu katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) kuendelea kuwa shakani.
Mfano halisi ni Shule ya Sekondari Temeke jijini Dar es Salaam yenye wanafunzi zaidi ya 2,600 wa kidato cha kwanza hadi cha sita , ambapo takribani 1,200 wanasoma masomo ya sayansi, lakini wana walimu 16 tu wa sayansi na fundi maabara mmoja.
“Licha ya kuwa shule yetu ni mchepuo wa sayansi upungufu wa vifaa na kemikali ni changamoto kubwa tunayokabiliana nayo kila siku,” anasema Innocent Mrutu ambaye ni mtaaluma mkuu na mwalimu wa somo la kemia katika shule hiyo.
Anasema pamoja na changamoto hiyo, katika hali ya kushangaza, idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita wanafanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho na kuchaguliwa kwenye vyuo vikuu mbalimbali nchini.
“Hapa tumefanikiwa kuondoa daraja sifuri na tumejiwekea malengo kila mwanafunzi atakayemaliza kidato cha sita, anapata ufaulu wa kwenda chuo kikuu ndiyo maana tunajitoa kwa kila namna kuhakikisha wanafunzi wetu wanaiva.
“Tatizo kubwa tulilonalo ni upungufu wa vifaa na kemikali kwa ajili ya majaribio, asilimia 80 ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita wanasoma sayansi hapo bado kuna wale wa madarasa ya chini, hii inasababisha hata hayo majaribio yafanyike kwa tabu,”anasema Mrutu.
Changamoto ya maabar ma vifaa vyake ni kubwa zaidi vijijini, ambapo baadhi ya wanafunzi wanalazimika kutumia maabara za shule jirani ili kufanya masomo ya vitendo.
Wadau mbalimbali waliozungumzia suala hilo wameeleza kuwa ili taifa lifanikiwe katika dhamira yake ya kuwa na uchumi wa viwanda na kizazi cha kisayansi, ni lazima kuwe na uwekezaji mkubwa katika elimu ya vitendo.
Wanashauri pia kuongeza idadi ya mafundi maabara, kuanzisha maabara za kidijitali pale inapowezekana, na kuhakikisha bajeti ya vifaa vya sayansi inalindwa dhidi ya kuhamishiwa kwenye matumizi mengine.
Wanasema bila vifaa na mazingira bora ya kujifunzia, ndoto ya kuibua wataalamu wa ndani wa kisayansi huenda ikabaki kuwa ndoto tu na sio uhalisia.
Mwalimu katika mojawapo ya sekondari mkoani Ruvuma John Mwakipesile anasema kwa sasa wanafunzi husoma kwa kusikia tu bila kuona au kugusa vifaa vya maabara.
Anasema katika shule nyingi, hasa za kata na za vijijini, walimu wanalazimika kufundisha masomo ya kemia, fizikia na baiolojia kwa nadharia pekee, bila kuwepo kwa mazingira ya kufanyia majaribio ya vitendo, jambo linalotajwa kuathiri kwa kiasi kikubwa uelewa wa wanafunzi.
“Kwa mfano, tunapofundisha somo la kemia kuhusu mchanganyiko wa tindikali wanafunzi hawajawahi hata kuona vifaa vya ‘test tube’ wala ‘bunsen burner’. Sayansi inakuwa kama sinema ya redio unasikia, lakini huoni,” anasema Mwakipesile.
Mchambuzi wa elimu, Dk Joyce Mhede, anasema upungufu wa maabara ni tatizo kuu linaloathiri matokeo ya masomo ya sayansi.
“Hatuwezi kutarajia wanafunzi wafanye vizuri katika fizikia, kemia au baiolojia bila kujifunza kwa vitendo. Mwanafunzi hawezi kuelewa matokeo ya jaribio la kisayansi kama hakushiriki kwa vitendo na hilo linahitaji maabara na vifaa,” anasema.
Juhudi zinazoendelea kufanyika
Tanzania kwa sasa inasukumwa na dhamira ya kujenga uchumi wa viwanda na wa maarifa kupitia elimu ya STEM. Hata hivyo, matokeo ya kitaifa yanaendelea kudhihirisha changamoto.
Katika mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2023, kiwango cha wanafunzi kufeli fizikia na kemia kilibaki juu ya asilimia 40, jambo linalohusishwa si tu na ubora wa ufundishaji, bali pia na uhaba wa rasilimali za maabara.
Aidha, ripoti ya BEST inaonesha kuwa ni asilimia 28 pekee ya shule zilizo na maabara ndizo zenye mafundi maabara waliobobea, hali inayowalazimu walimu wa sayansi kufanya kazi mbili za kufundisha na kuhudumia maabara.
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, mpango uliopo ni kuhakikisha kuwa shule zote za sekondari nchini zinakuwa na maabara zenye vifaa vya kisasa ifikapo mwaka 2030, ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaochagua masomo ya sayansi na teknolojia.
Mpango huo umeweka kipaumbele cha kujenga madarasa, kuimarisha elimu kidijitali, kuajiri walimu na kujenga maabara.
Katika bajeti ya mwaka 2025/26, sekta ya elimu imepangiwa Sh3.65 trilioni , sehemu ya fedha hizo zikielekezwa kwenye ujenzi na uboreshaji wa maabara.
Aidha, Serikali imetoa ufadhili kwa wanafunzi zaidi ya 1,000 mwaka huu ili kuhamasisha kusomea masomo ya STEM katika ngazi za juu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga, amewahi kusisitiza bungeni kuwa ushirikiano wa sekta binafsi, washirika wa maendeleo na taasisi za umma ni muhimu.
“Serikali haiwezi peke yake, tunahitaji wadau wote kuunga mkono juhudi hizi,” alisema.
HESLB yajitosa Temeke Sekondari
Hivi karibuni Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imechangia Sh10 milioni kwa Shule ya Sekondari Temeke ili kununua vifaa na kemikali muhimu kwa maabara ikiwa ni shehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Dk Bill Kiwia, anasema taasisi yake imeona umuhimu wa kushiriki moja kwa moja katika kuboresha elimu ya ngazi ya sekondari, kwa kuwa ndiyo msingi wa wanafunzi wa wengi wanaoomba mikopo ya elimu ya juu.
Anasema taasisi hiyo mara nyingi imekuwa ikihusishwa na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu pekee, ila imeona haiwezi kufanikisha jukumu letu bila kushirikiana katika hatua za awali za safari ya elimu.
“Ndoto yetu ni kila mwanafunzi wa Kitanzania kujifunza katika mazingira bora bila kujali anatoka wapi. Wanafunzi wanapokuwa na mazingira bora ya kujifunza masomo ya sayansi, itawasaidia kupata ufaulu mzuri na hatimaye kuwa wabunifu na wanasayansi bora,” anasema Dk Kiwia.
Anaongeza kuwa msaada huo ni sehemu ya mpango mpana wa taasisi hiyo kushirikiana na jamii kwa kuhakikisha elimu inakuwa jumuishi na yenye tija.
Mkuu wa shule hiyo, Ingia Mtenga, anasema msaada huo umekuja kwa wakati mwafaka kwani shule yake kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia masomo ya sayansi.