Dar es Salaam. Kwa miaka mingi kumejengeka dhana miongoni mwa Watanzania kuwa bidhaa zinazouzwa kwenye maduka ya kifahari ni halisi (original), huku zile zinazopatikana kwenye masoko ya kawaida yenye msongamano ni feki.
Si hivyo tu, wapo wanaoamini bidhaa ikiwa ghali ndiyo halisi. Lakini je, bei ndiyo kipimo cha ubora?
Mtazamo huo kwa muda mrefu umeathiri tabia za ununuzi. Mnunuzi kwenye duka la kifahari anaweza kulipa mara mbili ya bei ya viatu vya michezo vinavyopatikana Kariakoo, akiamini ananunua bidhaa halisi.
Hata hivyo, mara nyingi viatu vyote hivyo hutoka kiwanda kilekile, tofauti haipo kwenye ubora, bali gharama zilizoongezwa katika mnyororo wa usambazaji, zikiwamo za kodi za uingizaji, kodi za pango, gharama za chapa na masoko ambazo hupandisha bei.
Kwa mujibu wa mfanyabiashara wa simu, Salumu Abbasi, anayefanya biashara Makumbusho jijini Dar es Salaam, bei pekee haipaswi kutumika kama kipimo cha uhalisia wa bidhaa.
“Siyo kila mara kitu cha bei ghali ni original (halisi) na kinachouzwa kwa bei ya chini ni feki. Kuna maduka mjini yanayouza vifaa vya simu vilivyotumika, huku yakiwahadaa wateja kwamba ni vipya na havijafunguliwa. Ukweli ni kwamba vifaa hivyo si vipya, lakini vinauzwa kwa bei ya juu,” anasema.
Anasema kifaa kilekile kinaweza kupatikana Kariakoo kwa bei nafuu zaidi, huku muuzaji akiweka wazi kuwa kimetumika (mtumba), lakini bado kiko kwenye hali nzuri.
“Ni dhana tu imejengeka. Hususan kwenye vifaa vya kielektroniki, mara nyingi wateja huuziwa bidhaa feki au zilizotumika kwa bei kubwa wakiamini ni halisi, hata pale wanapopewa waranti,” anasema.
Kwa upande mwingine, mfanyabiashara eneo la Kariakoo, Khamis Kibwana, anasema katika eneo hilo mara nyingi bei za bidhaa ziko chini kwa sababu ya ushindani wa kibiashara unaotokana na wingi wa wafanyabiashara waliopo.
“Siyo kwamba ukienda Kariakoo au kwenye masoko mengine utauziwa bidhaa feki, hapana. Ukiona bidhaa inauzwa bei ya kawaida au ya chini, mara nyingi ina maana muuzaji ameamua kupunguza bei ili mzigo uishe haraka,” anasema.
Anasema Kariakoo yapo maduka yanayouza bidhaa kwa bei ghali na mengine ya chini, yakiwa na bidhaa feki na zile halisi.
“Hata kwenye maduka ya kifahari wapo wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoweza kukuuzia bidhaa feki. Tofauti pekee ni kwamba wanafanya biashara kwenye maeneo ya kifahari ambayo ni vigumu kwa wateja kuamini iwapo wanaweza kuuza bidhaa bandia,” anasema.
Muuza nguo Kariakoo, Fatuma Juma, anasema baadhi ya maduka yaliyo mjini huuza chapa zilezile kwa bei mara mbili akieleza: “Hapa Kariakoo tunauza kwa faida ndogo ili watu wengi zaidi wamudu. Ubora haupandi tu kwa sababu ya bei.”
Anasema Kariakoo wateja hupata chaguo linalolingana na bajeti zao bila kupoteza uimara wa bidhaa.
Mnyororo wa kimataifa wa usambazaji bidhaa umewezesha bidhaa kama vile viatu kutoka Uturuki au China kusafirishwa Tanzania na kupatikana madukani sehemu mbalimbali kwa bei tofauti.
Baadhi hupita kwa wasambazaji rasmi wenye maduka ya kifahari Oysterbay, vingine hupitia uagizaji wa jumla Kariakoo. Bidhaa ya mwisho inaweza kuwa ileile, lakini kinachoelezwa kuihusu ndicho hubadilisha mtazamo wa mteja.
Maduka ya kifahari huuza kwa mtazamo wa upekee wa bidhaa, huku Kariakoo huuza kwa kuangalia unafuu wake. Kinachobadilika si bidhaa yenyewe kila mara, bali kinachoelezwa juu yake.
“Wazazi wetu walitufundisha vitu halisi lazima viwe ghali, lakini siku hizi wateja wanajifunza kwamba hilo halina ukweli wakati wote,” anasema Jumanne Ramadhani na kuongeza kuwa mara nyingi unacholipia kwenye maduka ya kifahari ni ufungaji mzuri na kiyoyozi.
Mama wa watoto watatu, mkazi wa Sinza, anashuhudia hilo kupitia vifaa vyake vya jikoni.
“Nilinunua blenda mjini kwa Sh250,000, iliharibika ndani ya miezi mitatu. Lakini ile niliyoinunua baadaye Kariakoo kwa nusu ya bei imedumu miaka miwili. Hapo ndipo nilipojifunza kwamba bei siyo kila mara kipimo cha ubora,” anasema.
Anasema hata maduka ya kifahari yanaweza kuuza bidhaa bandia, tofauti pekee ni kuwa maeneo yao ya biashara huwafanya wateja wasiwe na shaka.
Khadija Kibwana anasema gharama za chini za bidhaa kwenye masoko makubwa kama Kariakoo mara nyingi huonesha ushindani, siyo bidhaa feki.
“Ukiiona bidhaa kwa bei nafuu, mara nyingi inamaanisha muuzaji anataka kumaliza mzigo haraka,” anasema akieleza watu wengine hupenda maduka ya kifahari kwa sababu ya urahisi wa kuyafikia na muonekano wake.
Kwa wafanyabiashara, mabadiliko ya kimtazamo ni fursa kwao. Wanaoshikilia dhana kuwa ghali ndiyo halisi wanaweza kujikuta wakihangaika, wakati wajasiriamali wanaoonesha ubora kwa uwazi na uaminifu wakipata nafasi kubwa katika mauzo.
Katika soko la Tanzania la leo, bei si kila mara kipimo cha ubora. Iwe imenunuliwa Kariakoo, Masaki au mtandaoni, kipimo halisi cha uhalisia wa bidhaa siyo bei, bali bidhaa yenyewe.