Makocha wazawa waichunia Simba | Mwanaspoti

Wakati uongozi wa Simba ukianza kupokea maombi na wasifu wa makocha mbalimbali kwa ajili ya kumrithi Kocha Mkuu, Fadlu Davids aliyeamua kutimkia Raja Casablanca, hadi sasa hakuna kocha mzawa aliyeomba nafasi hiyo.

Hilo linatokea huku kocha huyo akiiaga klabu hiyo huku akijiunga na rasmi na Raja Casablanca ya Morocco.

Tangu juzi mara baada ya kuwepo na uhakika kuwa Fadlu hatorejea Simba, makocha mbalimbali kutoka nje na ndani ya bara la Afrika wameonekana kuchangamkia fursa ya kurithi mikoba ya kocha huyo raia wa Afrika Kusini lakini kati ya hao, hakuna mwenyeji aliyeonyesha uthubutu wa kuhitaji nafasi hiyo.

Chanzo cha uhakika ndani ya Simba kimefichua kuwa tayari mchakato wa kumpata kocha mpya umeshaanza lakini hakuna mwitikio kwa makocha wa nyumbani.

“Maombi yameshaanza kutumwa na makocha mbalimbali na miongoni mwao wapo wenye majina na uzoefu mkubwa wa soka la Afrika lakini hatujaona maombi kutoka kwa makocha wazawa labda tusubiri labda yanaweza kutufikia.

“Suala la kutafuta kocha mpya litafanyika kwa haraka kwa sababu muda uliobakia kabla ya mechi ya marudiano na Gaborone United ni mfupi na timu inahitaji kuwa na msimamizi wa benchi la ufundi mapema kabla msimu haujaanza kuchanganya,” kilifichua chanzo hicho.

 Jana Fadlu aliiaga klabu hiyo na muda mfupi baadaye alitambulishwa na Raja.

“Ni kwa moyo mzito naiaga Simba SC. Tangu nilipowasili, nilihisi shauku ya klabu hii kubwa na upendo wa mashabiki wake wa ajabu. Pamoja tulipigana, tukasherehekea na tukaimarika kupitia kila ushindi na kila changamoto. Shukrani zangu za dhati kwa Rais MO Dewji kwa uongozi wake wa kutia moyo, maono na usaidizi wake wa kudumu.

“Kwa wachezaji, endelea kupigana, endelea kuamini, na endelea kuinua beji kwa heshima.

Kwa wafanyakazi na wasimamizi, asante kwa uaminifu wako na kujitolea bila kuchoka nyuma ya pazia.

“Kwa mashabiki wa Simba, nyinyi ndio mapigo ya moyo wa klabu hii. Sauti zenu, nyimbo zenu, shauku yenu isiyoyumba itasikika katika kumbukumbu zangu. Asante kwa kuikaribisha familia yangu kuwa yenu. Simba daima itakuwa sehemu yangu na ninaitakia klabu mafanikio na vikombe mbeleni. Asanteni Sana, forever Nguvu Moja,” amesema Fadlu Davids.

 Baada ya Fadlu kuaga, Raja Casablanca ilitangaza rasmi urejeo wake kama Kocha Mkuu huku Simba nayo ikimuaga.

“Klabu ya Simba inamshukuru Kocha Fadlu kwa kuiongoza Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kumalizia nafasi ya pili kwenye Ligi kuu ya NBC.

Uongozi wa klabu unamtakia kheri na baraka kocha Fadlu katika maisha yake ya soka nje Simba,” ilifafanua taarifa hiyo ya Simba.