Mjane, Alice Haule na binti yake amekwenda Kituo cha Polisi, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, kutokana na nyumba yake iliyoko Mikocheni kuvamiwa na watu waliodai walikuwa wakimdai hayati mume wake.
Watu hao walimuondoa kwa nguvu ndani ya nyumba hiyo mchana wa leo Septemba 23, 2025, huku wakimuonyesha barua iliyodaiwa imetoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kinondoni ilikitoa maelekezo kwa kampuni ya udalali kumuondoa katika nyumba hiyo.
Mbali ya Alice, wapangaji wengine katika nyumba hiyo pia wameondolewa.
Kutokana na tukio hilo, Dk Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram ameandika:
“Asante kwa ushirikiano, mama mjane amenitumia sms, nikampigia, nikamsikiliza. Kifupi amesema, mwanasheria anaye, kesi iko Polisi na pia Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni anajua jambo hili.”
“Hata hivyo, changamoto zilizotokea ni huko kuvamiwa ghafla bila taarifa na kinyume na utaratibu stahiki wa kisheria ukizingatia kuwa, kesi iko Polisi. Hivyo, msaada wa haraka anaohitaji ni ulinzi wake na mali zake na dhidi ya hayo matishio anayopata,” ameandika Dk Gwajima.
Kuhusu hatua alizochukua amesema amewasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na RPC Kinondoni na kuomba, wafanye hatua stahiki ili mama mjane kwanza awe salama na utulivu kisha, hayo ya kisheria yaendelee kwa mujibu wa sheria ambapo, viongozi wote hao wamepokea kwa hatua stahiki.
“Aidha, saa 9:11 jioni nimeongea tena na mama mjane ambapo, ameniambia ni kweli Polisi walienda na wale waliokuwa wanamfanyia vurugu walitawanyika na sasa hali iko kwenye utulivu,” ameandika.
Dk Gwajima ametoa wito kwa wanaodai kununua nyumba ya mjane akisema:
“Ndugu, hata kama mnadaiana, tafadhali fuateni taratibu halali za kisheria kupitia kwa mwanasheria wa mjane huyu. Hata katika mapito ya kisheria, tafadhali kumbukeni kuwa na subira na utu uwe kwanza na hapo ndiyo kila mmoja atapata haki yake na Mwenyezi Mungu atapendezwa nanyi nyote na kuwabariki wote. Amina.”
Amesema: “Tuendelee kushirikiana kuzuia changamoto za kijamii na kuibua zinapotokea na kuzipatia mwongozo stahiki kwa wakati.”
Endelea kufuatilia Mwananchi Digital.