Mmoja wa wanaodaiwa kuchepusha fedha Tamisemi, ajisalimisha kwa DPP

Dar es Salaam. Aliyekuwa mkuu wa kitengo cha udhibiti taka na usafi wa mazingira wa Manispaa ya Kigamboni, Juvenalis Mauna (53) amemwandika barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), akiomba kukiri na apunguziwe adhabu ili aweze kuimaliza kesi yake.

Mauna ni mshtakiwa wa tatu katika kesi ya kuchepusha fedha na kuisababishia Tamisemi hasara ya Sh165 milioni.

Mshtakiwa huyo na wenzake 12 wanakabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo, kutakatisha fedha na kuongoza genge na kufanya ubadhilifu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali, Eric Davies ameieleza Mahakama hiyo, leo Jumanne, Septemba 23, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upande wa mashtaka wamewasilisha kibali cha kuruhusu kesi hiyo ya uhujumu uchumi kusikilizwa mahakamani hapo.

Wakili Davies alitoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.

“Upelelezi wa kesi hii umekamilika na tupo katika hatua za kusajili taarifa na nyaraka muhimu kwa ajili ya kesi hii pamoja na kuandaa kibali cha kuruhusu isikilizwe,” amesema  Davies na kuongeza;

“Pia, ofisi imepokea barua ya mshtakiwa wa tatu katika kesi hii (Mauna) akiomba kufanya majadiliano na DPP, hivyo barua hiyo tunaifanyia kazi na tutamjibu,” amesema Davies.

Baada ya kueleza hayo, aliomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya hatua zaidi. Hakimu Swallo ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 30, 2025.

 Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa mkuu wa idara ya fedha na mhasibu wa Manispaa ya Kigamboni, Jonathan Manguli (38).

Wengine ni aliyekuwa mhasibu wa manispaa hiyo Godfrey Martiny (44), mkuu wa kitengo cha udhibiti taka na usafi wa mazingira wa manispaa hiyo, mhandisi Josephat Mutembei ( 39) na ofisa ugavi msaidizi wa manispaa huyo, Bibiana Mdete (53).

Pia, yupo, aliyekuwa ofisa ugavi, Henry Rugayi (38), mhasibu Annie Maugo (43), ofisa hesabu kutoka Tamisemi Dodoma, Tumsifu Christopher (46) na ofisa hesabu, Aidan Mpozi (61) wote kutoka Manispaa ya Kigamboni.

Wengine ni wafanyabiashara Hamis Manfred (40), Paulo Mwakyusa (43), Godwin Cheyo (33) na Jennifer Manguli(30).

Kati ya mashtaka hayo 10; matatu ni ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumpotosha mwajiri wao, mawili ni ya kuongoza genge la uhalifu, mawili ni ya ubadhirifu wa fedha, moja ni kuchepusha fedha, kutakatisha fedha na kuisababishia hasara Tamisemi.