KOCHA Hemed Suleiman ‘Morocco’ amewasili jijini Dar es Salaam, tayari kwa kupokea jukumu jipya la kuifundisha Simba kwa muda, huku akifunguka kazi atakayokutana nayo.
Morocco, amewasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere leo asubuhi, akitokea nyumbani kwake Zanzibar, ikiwa ni siku moja tangu jana usiku atangazwe kuwa kocha wa Wekundu hao.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Morocco amesema, haikuwa rahisi kukubali jukumu hilo lakini ametaja weledi ndio umemfanya akubaliane na ajira hiyo ya muda.
Morocco ambaye pia ni kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, amesema anakwenda kukutana na viongozi wa Simba, kisha baada ya hapo ataanza mara moja kazi hiyo.
“Nimefika salama namshukuru Mungu, ninachoweza kusema nakwenda kukabiliana na changamoto nzuri, lakini ina ugumu wake,” amesema Morocco ambaye amewahi kuzifundisha klabu za Namungo, Geita na Coastal Union.
“Haikuwa rahisi kukubalina na hili jukumu, unajua mimi bado ni kocha wa timu ya taifa, lakini baada ya kuzungumza na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) maana wao ndio waajiri wangu walikubali kunipa hiyo nafasi.
“Nimetanguliza weledi kwenye kuamua hili, nakwenda Simba ni timu kubwa, nahitajika kwenda kutuliza presha ya wafuasi wake wengi ambao wanatarajia kuona timu yao inatulia.
“Nakwenda kujiunga na timu ambayo sikufanya usajili na ipo kwenye mashindano, lakini pia haikuwa na utulivu mkubwa, nampongeza kocha aliyetangulia Fadlu (Davids) ni rafiki yangu amefanya kazi yake nzuri na ameondoka, nadhani ni hatua ya kuanzia hapa alipoishia na kwenda mbele.”
MUDA ALIOPEWA SIMBA
Morocco amesema kuwa, ametua Simba kwa ajili ya kuchukua nafasi ya muda mfupi, wakati klabu inasaka kocha mpya atakaekuja kukiongoza kikosi hicho msimu huu wa 2025/26.
“Nimetua Simba kuja kuchukua nafasi ya muda kuifundisha timu hiyo, baada ya Fadlu kusitisha ajira yake, hivyo nipo kwa ajili ya mechi chache zijazo hasa kimataifa.”