Mwalimu aahidi kujenga Kariakoo ndogo Nkasi

Nkasi. Ili kukuza uchumi wa wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani na kuimarisha fursa za kibiashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimeahidi kuanzisha soko la biashara la ‘Kariakoo ndogo’ katika Kijiji cha Kirando, wilayani Nkasi, Mkoa wa Rukwa endapo kitachaguliwa kuunda Serikali Jumatano ya Oktoba 29, mwaka huu.

Chama hicho kimesema ujenzi wa soko hilo litakalojengwa kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika, hautaathiri Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, bali utalipunguza mzigo na kuongeza mzunguko wa uchumi katika maeneo ya pembezoni hasa wanaoishi mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Akizungumza leo Jumanne Septemba 23, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Kirando, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chaumma, Salum Mwalimu amesema ujenzi wa Kariakoo hiyo utarahisisha upatikanaji wa bidhaa muhimu kwa wananchi wa pande zote mbili za mpaka sambamba na kupunguza gharama za usafiri kwa wafanyabiashara wa DRC, hali itakayosaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Tanzania.

“Ondoa msongamano Kariakoo, tengeneza Kariakoo nyingine Kirando. Wapunguzie Wa-Congo gharama za kusafiri hadi Dar es Salaam. Leo mtu anatoka Congo anatembea siku tatu hadi Kariakoo, lakini akija Kirando ni saa nne tu,” amesema Mwalimu.

Amesema soko hilo litaleta mapinduzi ya kiuchumi kwa mikoa ya mipakani, hasa maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika huku akishutumu ukiritimba na sera zisizo rafiki kwa biashara kama sababu ya wananchi kushindwa kunufaika na fursa zilizopo.

“Kwa nini vijana wa Kenya wanakuja Tanzania kuchukua mpunga, mahindi, parachichi na kuwa matajiri, lakini sisi tunawafungia vijana wetu fursa hizo? Kirando ina nafasi ya kuwa lango kuu la kiuchumi kwa DRC,” alisema mgombea huyo.

Mwalimu amesema Chaumma ikichukua dola, itajenga miundombinu ya kisasa eneo la Kirando ikiwamo bandari ndogo na usafiri wa meli, ili kuwezesha usafirishaji wa bidhaa kwenda Congo kwa urahisi.

Mwalimu amesema hatua hiyo itaongeza thamani ya uzalishaji wa ndani na kupanua wigo wa masoko kwa bidhaa za Tanzania.

Awali, katika mkutano huo, Haipolito Kaninga, mgombea ubunge wa Nkasi Kaskazini kupitia Chaumma aliahidi akichaguliwa kuwa mbunge, atapigania kufunguliwa kwa mpaka wa Kirando ili kuimarisha uchumi wa eneo hilo na kuchochea ushirikiano wa kibiashara na DRC.

Kaninga amesema eneo hilo lina nafasi kubwa ya kiuchumi kutokana na ukaribu wake na DRC, wananchi wengi kutoka upande wa nchi hiyo hasa mwambao wa ziwa hilo, hufika Tanzania kwa ajili ya kununua mahitaji yao ya kila siku katika maeneo ya Kirando, Kabwe na Kapili.

“Raia wengi wa Congo wanakuja kuchukua bidhaa Kirando kwa sababu tuko karibu. Usafiri kwa boti ni saa nne tu. Serikali ikifungua rasmi mpaka huu, uchumi wa wananchi utaimarika,” amesema Kaninga.