Dar es Salaam. Mwili wa Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga umeagwa, akikumbukwa kama mpenda haki na usawa kwa jamii.
Dk Munga amefariki dunia Jumamosi, Septemba 20, 2025, saa 9:30 usiku akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rabinisia, jijini Dar es Salaam.
Ibada ya kumuombea na kuaga mwili wa Dk Munga imefanyika leo Septemba 23, 2025 katika Kanisa la KKKT Usharika wa Kunduchi Beach. Imehudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, Serikali na vyama vya siasa.
Ibada hiyo imeongozwa na Mkuu wa Kanisa la KKKT, Dk Alex Malasusa.

Dk Malasusa amemzungumzia Askofu mstaafu Munga akisema ameacha alama isiyosahaulika katika maisha ya watu.
Amesema katika uhai wake aliishi kwa upendo na kumtumikia Mungu, akiwa mstari wa mbele katika masuala ya kijamii.
“Tunaendelea kumshukuru Mungu kwa ajili ya maisha yake na mambo mema ambayo ameyafanya. Hakika tutaendelea kuyaenzi,” amesema.
Amewahimiza waumini kulishika neno la Mungu, kuishi katika utakatifu, uaminifu na kumjua Mungu ili kuuona ufalme wake na kuvikwa taji la uzima.
Dk Malasusa amesema hakutakiwi kuwa na muda maalumu wa kutekeleza hayo au kuyafanya katika sehemu ya ibada pekee, bali iwe ni sehemu ya maisha ya kila siku hadi kifo.
“Kifo siyo kupotea bali ni mwanzo wa maisha mengine ya pumziko, ukisubiri ufufuo,” amesema.
Dk Malasusa amewakumbusha wazazi umuhimu wa kutenga muda wa malezi kwa watoto wao akitoa mfano wa Dk Munga namna alivyolizingatia hilo na upendo kwa watoto.
Amewataka kuacha visingizio vya wingi wa majukumu ya kazi, kwani uwepo wao ni muhimu katika ukuaji wa mtoto.

“Tunaona walivyomuelezea Askofu (Munga) namna alivyokuwa anatenga muda kwa ajili yao na kuwalea watoto kwa upendo na mimi nimeshuhudia, kina baba wengi hatufanyi hivi kwa kisingizio tuko ‘bize’ na kazi. Tenga muda wa kuwa na watoto wako,” amesema.
Kwa upande wake, mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba, amesema Askofu Munga alipenda kuona haki na usawa unatawala katika jamii.
Amesema hiyo ni moja ya sababu iliyowezesha Askofu Munga baada ya kustaafu kuanzisha taasisi inayoshughulika na masuala ya haki, amani na suluhu katika jamii (IPR) ambayo amesema ilisajiliwa mwaka 2019.
“Nikiwa Mwenyekiti wa Bodi wa taasisi hiyo nitahakikisha tunayaenzi maono aliyotuachia,” amesema.
Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Carlotta Macias amesema hatasahau ukarimu na upendo aliooneshwa na Askofu Munga na mkewe miaka mitatu iliyopita alipotembelea eneo la Maramba, mkoani Tanga.
Marehemu Askofu mstaafu Munga atazikwa eneo hilo kesho Septemba 24, 2025.
Mwanadiplomasia Carlotta amesema Dk Munga ni chemchemi ya hekima na busara, akiwa mfano wa mtu mwenye upendo kwa jamii.
“Kuondoka kwake kunaacha pengo ambalo ni ngumu kuzibika, lakini kumbukumbu ya mema aliyofanya itaishi daima kwa wale aliyowagusa maisha yao,” amesema.
Dk Munga amezaliwa Machi 6, 1955 katika Kijiji cha Tewe wilayani Lushoto, mkoani Tanga akiwa mtoto wa saba kati ya watoto tisa.
Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Tewe mwaka 1961 hadi 1967.
Elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Old Moshi na Tambaza 1969-1971 kisha akajiunga na Chuo cha Theolojia Makumira 1982-1984.

Baadaye alikwenda Sweden kuendelea na masomo akapata Shahada ya Uzamivu katika Theolojia.
Alifunga ndoa na Aneth Magawa, Aprili 6, 1986 katika Kanisa la KKKT lililoko Maramba.
Askofu Munga amehudumu Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki mwaka 2001 hadi 2022.