Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema kuwa endapo atachaguliwa kuongoza dola ataanzisha mfuko maalumu wa maisha ya mwalimu, ili kuwaondolea utegemezi wa mikopo yenye masharti magumu na isiyokuwa na tija kwa maisha yao.
Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, amesema hayo leo Jumanne Septemba 23,2025 katika mkutano wake wa hadhara wa kampeni za urais uliofanyika Jimbo la Bububu Mkoa wa Mjini Unguja.
Katika maelezo yake, Othman amesema kada ya ualimu bado inadharaulika Zanzibar, lakini chini ya serikali ya ACT-Wazalendo itakaposhika dola itawaheshimisha walimu wote wa visiwa hivyo.
“Mwalimu ndio macho yetu, ndio jicho la Taifa, mwalimu ndiye anawazalisha marais, madaktari, mawaziri, wabunge na viongozi mbalimbali. ACT tutatazama heshima yao, kuanzia mafunzo, haki na masilahi yao,” amesema Othman.
Ili kufanikisha hilo, Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, amesema wataunda tume ya utumishi ya walimu itakayosimamia masilahi yao ikiwemo, likizo na mahitaji mengine.
“Tutakwenda kunyanyua heshima ya mwalimu kuangalia masilahi yake, si mshahara tu bali yote yanayomhusu, tutakomesha mwalimu kupewa mikopo ya kausha damu, tutawaanzisha mfuko wa kuendesha maisha ya mwalimu.”
“Utaratibu huu utakomesha mwalimu kukopa Sh10 milioni akalipishwa Sh16 milioni. Tunataka mwalimu akikopa Sh10 milioni basi alipe Sh10.5 milioni, huu ndio mwarobaini wa mikopo kausha damu,” amesema.
Katika kuboresha sekta ya elimu visiwani humo, Othman amesema ataufumua mfumo wa elimu wa Zanzibar ili kuendana na mahitaji halisi ya wanafunzi wa visiwa hivyo.
Amedai mfumo wa sasa wa elimu si rafiki kwa wanafunzi wa Zanzibar, unawachanganya akitolea mfano mtu anayemaliza kidato cha sita hivi sasa hajui kilichomo ndani ya bahari na mazingira yake.
“Leo tuna wanafunzi watakueleza kuhusu volcano, lakini hajui kuhusu bahari wakati ndio uchumi wa Zanzibar. Tutaupanga mfumo wa elimu ili kuendana na mahitaji ya Zanzibar,” amesema Othman.
Amesema sera ya elimu iliyopo katika ilani ya uchaguzi wa ACT-Wazalendo, itahakikisha inatambua mahitaji ya sekta hiyo ili wanafunzi kupata elimu bora iliyosheheni maarifa na jambo hilo, ndilo litakaloamua kuhusu mitaala ya Zanzibar.
Mwenyekiti wa kamati ya ushindi ya ACT- Wazalendo, Ismail Jussa amesema endapo Othman akifanikiwa kushinda uchaguzi Oktoba 29, atawaonyesha kwa vitendo namna serikali inavyoweza kulipa mshahara wa Sh1 milioni kima cha chini kwa watumishi wa umma.
“Atawaonyesha namna ya uchumi wa Zanzibar unavyoweza kupaa si kwenye karatasi bali katika maisha ya wananchi,” amesema Jussa.
Mwenyekiti wa mkoa wa kichama wa Magharibi A, Raisa Bakari amesema Othman ni kiongozi anayetetea haki za wananchi waliodhulumiwa wakimfananisha na msanii nyota wa tamthilia ya kituruki ya ‘The Ottoman’.