SHULE YA MSINGI MPAKANI YAPATA MSAADA WA MATANKI YA MAJI SAFI KUTOKA ANGLE PARK.


 Dar es Salaam – Uongozi wa Angle Park umeeleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kusaidia kutatua changamoto zinazozikabili shule za msingi na sekondari, hususan zilizoko katika maeneo jirani na makazi yanayozunguka kampuni hiyo.

Akizungumza katika makabidhiano kwa uongozi wa Shule ya Msingi Mpakani, Mkurugenzi wa Angle Park, Bonifasi Daniely, amesisitiza kuwa elimu ndiyo nguzo ya maendeleo ya jamii, hivyo mshikamano kati ya sekta binafsi na wadau wengine ni muhimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Katika tukio hilo, kampuni imetoa matanki mawili ya lita 3,000 kila moja ya kuhifadhi maji safi, yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.2.

“Angle Park itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha tunapunguza changamoto za shule zetu. Elimu kwanza,” alisema Daniely.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mpakani, Ruchana Mhapa, ameishukuru Angle Park kwa msaada huo na kueleza kuwa utasaidia kwa kiwango kikubwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi shuleni hapo.

“Msaada huu ni ukombozi mkubwa kwetu. Awali wanafunzi walikuwa wakipata changamoto ya maji, hasa wakati wa vipindi vya usafi na matumizi ya kila siku. Tunawashukuru Angle Park kwa kutuunga mkono, kwani jitihada zao zinaboresha mazingira ya kujifunza na kufundisha,” alisema Mwalimu Mkuu.

Wadau wa elimu wamepongeza jitihada hizo na kusisitiza kuwa msaada wa pamoja kutoka kwa mashirika na jamii ni chachu muhimu ya kuinua kiwango cha elimu nchini