Dar es Salaam. Dalili za uhuru wa Palestina zazidi kuonekana, kufuatia uungwaji mkono wa karibu mataifa 150, ikiwemo nchi nne zenye kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambazo sasa zimetambua rasmi taifa hilo.
Chini ya Mkataba wa Montevideo wa mwaka 1933, kuna vigezo ili Palestina itambuliwe kuwa taifa huru chini ya sheria ya kimataifa, inahita kukidhi vigezo kdhaa.
Licha ya kutosaini Mkataba wa Montevideo wa mwaka 1933, Uingereza imetangaza rasmi kulitambua taifa la Palestina, na kuadhimisha hatua hiyo kwa kuzindua ubalozi wake jijini London, ambapo bendera ya Palestina ilipandishwa wiki hii kwa mara ya kwanza.
Taifa la Palestina limetambuliwa rasmi na mataifa 151 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na zaidi ya nchi 12 kutoka barani Ulaya, zikiwemo Hispania, Ireland na Norway.
Hata hivyo, ili Palestina iwe mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa inatakiwa ithibitishwe kwa angalau kura tisa za wajumbe wa Baraza la Usalama na si kura ya veto.
Baraza la Usalama lina wajumbe 15, huku watano wakiwa wa kudumu ambao ni Uingereza, Marekani, Ufaransa, Russia na China.
Kwa sasa, wajumbe 10 wa muda wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha miaka miwili ni Algeria, Denmark, Ugiriki, Guyana, Pakistan, Panama, Jamhuri ya Korea, Sierra Leone, Slovenia na Somalia.
Miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Usalama, nchi ambazo tayari zimetangaza kuunga mkono kutambuliwa kwa taifa la Palestina ni nchi 11 za Somalia, Guyana, Slovenia, Algeria, Pakistan, Sierra Leone, China, Ufaransa, Urusi na Uingereza.
Marekani imepinga waziwazi, huku Ugiriki na Denmark zikieleza kuwa bado haziko tayari kwa hatua hiyo, na Panama haijatoa msimamo wake rasmi hadi sasa.
Ikiwa Baraza la Usalama litakubali ombi hilo, litapelekwa kwenye mkutano wa Baraza Kuu kwa uidhinishaji ambapo inahitaji kura ya theluthi mbili ya wanachama wote 193.
Kwa hivyo, ndani ya Baraza la Usalama, taifa huru la Palestina limeungwa mkono na nchi 11, likivuka kiwango kinachohitajika cha nchi tisa.
Aidha, katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ili taifa la Palestina litangazwe kuwa huru, inahitajika theluthi mbili ya nchi wanachama 193, sawa na nchi 128.
Kwa sasa, takriban nchi 150 zimeonyesha kuunga mkono jitihada hiyo.
Kuanzia mwaka 1988, takriban mataifa 81, yakiwemo China na Russiaq, yalitambua rasmi taifa huru la Palestina.
Idadi hiyo imeendelea kuongezeka hadi sasa, ambapo Uingereza na Ufaransa ni miongoni mwa nchi zilizotoa uungwaji mkono wao mwaka huu.
Maana ya tamko la Uingereza
Tangazo la Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer kutambua taifa ya Palestina ni kukubali haki zote za kisheria na wajibu wa utawala wa taifa hilo jipya ikiwamo kuleta suluhisho la amani kati ya mataifa mawili ya Palestina na Israel.
Kwa maana hiyo Serikali ya Uingereza sasa inaitaja Ukanda wa Magharibi (West Bank) na Gaza kama Palestina badala ya “Occupied Palestinian Territories”, na imefanya mabadiliko hayo kwenye tovuti yake.
Pia, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imebadilisha ramani ya ushauri wa kusafiri kwa eneo hilo, ikitumia jina Palestina.
Uamuzi huu unamaanisha Palestina itapata haki kamili za kidiplomasia na ofisi rasmi ya balozi kwa upande wa Uingereza ambayo tayari imefunguliwa Jumatatu jijini London.
Wazari ya Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper, tayari ametoa taarifa kuandika barua kwa mwenzake wa Palestina wakati unaofaa kuweka wazi taratibu za kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.
Kabla ya tamko hilo ujumbe wa Mamlaka ya Palestina Uingereza haukuwa katika kiwango cha ubalozi na unafanya kazi kama “mission ya kidiplomasia” makao yake iko Hammersmith, magharibi mwa London.
Kwa maana hiyo hadhi ya ubalozi kwa Palestina itawezesha kupata haki ya ulinzi na haki maalumu chini ya Mkataba wa Vienna.
Serikali ya Palestina ina sheria ya kujitawala sehemu katika Ukanda wa Magharibi chini ya makubaliano na Israel, inatoa pasipoti za Palestina, na inaendesha mifumo ya afya na elimu kwa sehemu hizo.
Lakini, bado kuna vizuizi kama biashara, uwekezaji, masomo na utamaduni vimezuiwa kwa sehemu na Israel.
Hakuna uwanja wa ndege wa Palestina kwa sasa na Ukanda wa Magharibi hauwezi kufikiwa bila kupitia Israel au mpaka unaodhibitiwa na Israel kuelekea Jordan.
Gaza pia iko chini ya upatanishi wa Israel kwa njia ya utawala na usalama.
Sehemu kubwa ya ardhi ambayo ingeweza kuwa taifa la Palestina imekuwa chini ya ukoloni wa kijeshi wa Israel kwa zaidi ya miaka 50.
Kauli ya Waziri Mkuu Starmer ni kwamba wakati wa kutambua Palestina ni sasa, kwani matumaini ya suluhisho la mataifa mawili (Israel yenye usalama na Palestina yenye uwezo) yanaonekana kutoweka.
Stamer anasema hiyo ni sehemu ya mpango wa hatua nane uliokubaliwa na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.
Uingereza ilisema kutambua Palestina utatekelezwa ikiwa Israel haitatimiza baadhi ya masharti kama kusitisha mapigano, kuruhusu misaada ya kibinadamu ipitie, na kuacha mipango ya unyonyaji wa ardhi.
Kwa mujibu wa Starmer Uingereza inatambua haki isiyoweza kubebwa ya watu wa Palestina na kile anachokiona kama jukumu la kimaadili la kuendelea kuweka suluhisho la mataifa mawili hai, katikati ya uharibifu wa vita na wasiwasi kuhusu upanuzi wa makazi huko Ukanda wa Magharibi.
Mwaka 1947, Umoja wa Mataifa ulipitisha Azimio la 181 lililogawanya Palestina kuwa mataifa mawili moja kwa Wayahudi na lingine kwa Waarabu. Hata hivyo, mpango huu haukukubaliwa na nchi za Kiarabu, na vita vilizuka baada ya kuundwa kwa taifa la Israel mwaka 1948.
Tangu wakati huo, mvutano kati ya Wapalestina na Waisraeli umeendelea kuongezeka, ukichochewa na vita vikubwa kama vile Vita ya Kiarabu na Israeli ya mwaka 1948, Vita ya Siku Sita ya mwaka 1967, na intifada kadhaa.
Zaidi ya hayo, maelfu ya Wapalestina, wakiwemo watoto, wamezuiliwa au kufungwa kwa sababu mbalimbali.
Ujenzi wa makazi haramu ya Israel katika maeneo ambayo yanapaswa kuwa sehemu ya taifa la Palestina umezidisha zaidi hali ya sintofahamu, kwa kupunguza ardhi ya makazi na kuvuruga maisha ya watu wetu walioko huko.