Tanzania Yazindua Matokeo ya Tathmini ya Kitaifa ya Hatari za Mabadiliko ya Tabianchi

 


Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kwa kushirikiana na Shirika la Mitaji ya Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCDF) kupitia Programu ya LoCAL, na kwa msaada wa Umoja wa Ulaya, Norway, Ubelgiji na Ireland, imezindua rasmi ripoti ya kwanza ya aina yake ya Tathmini ya Hatari na Uwezekano wa Kuathirika na Mabadiliko ya Tabianchi (CRVA) katika ngazi ya halmashauri za Tanzania Bara na Zanzibar.

Ripoti hiyo inabainisha maeneo yenye hatari kubwa ya kuathirika na mabadiliko ya tabianchi, viwango vya kuathirika, pamoja na uhitaji wa uwekezaji wa haraka na wa kimkakati ili kujenga ustahimilivu wa jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwakilishi wa Ofisi ya Rais, Eng. Emmanuel Enock Nyanda, kwa niaba ya Katibu Mkuu OR-TAMISEMI amesema wanawashukuru UNCDF, Umoja wa Ulaya, Norway, Ubelgiji na Ireland kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutambua maeneo hatarishi na kuainisha mbinu za ustahimilivu. Matokeo ya tathmini hii yatawawezesha watunga sera, viongozi wa halmashauri, na wananchi kupanga na kutekeleza hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kilimo na ufugaji unaozingatia mabadiliko ya hali ya hewa.”

Changamoto Kubwa za Tabianchi

Pia amesema kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto za ongezeko la joto, ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko na kuongezeka kwa kina cha bahari. Sekta muhimu kama kilimo, utalii, uvuvi, nishati na miundombinu ya maji zipo hatarini, na tafiti zinaonyesha kuwa bila hatua madhubuti, mabadiliko haya yanaweza kugharimu hadi 4% ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2050, na kupeleka mamilioni ya wananchi kwenye umasikini zaidi.

Wito wa Wadau

Naye Mwakilishi wa wafadhili wa Programu ya LoCAL amesema badala ya kufanya maamuzi kwa kubahatisha, sasa wana taarifa sahihi na za kisayansi. Hii itahakikisha kila shilingi inayotumika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inawanufaisha zaidi wananchi walio hatarini na kulinda mustakabali wa taifa.”

“Ufadhili bila maarifa ni kupoteza rasilimali. Ripoti hii ya CRVA inatoa maarifa ya kisayansi, na UNCDF kupitia LoCAL tunaendelea kujengea uwezo halmashauri ili kujenga ustahimilivu wa jamii.” Alisema Mwakilishi wa wafadhili wa Programu ya LoCAL

Pia alibainisha vipaumbele vya uwekezaji na tathmini hiyo imependekeza hatua za kujenga ustahimilivu wa mijini ikiwemo ujenzi wa mifereji ya kudhibiti mafuriko na kupunguza athari za joto, kulinda bioanuwai ya ukanda wa pwani kupitia urejeshaji wa mikoko na maeneo oevu, kuboresha usalama wa maji kupitia ukarabati wa vyanzo na miundombinu ya hifadhi ya maji, kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, pamoja na kukuza uchumi jumuishi kupitia kilimo chenye mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na bima kwa wakulima wadogo hususan wanawake.

Tangu kuanzishwa mwaka 2018, Programu ya LoCAL imekuwa ikitekelezwa katika halmashauri 3, na sasa inalenga kufikia halmashauri 21 kote nchini kwa msaada wa washirika wa maendeleo.