Dar es Salaam. Wataalamu 29 wa ukuzaji mitaala kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) wamehitimu mafunzo maalumu ya miezi mitatu yaliyoratibiwa na Aga Khan Education Services Tanzania.
Lengo la mafunzo hayo ni kuboresha utoaji wa elimu shuleni na kuwawezesha wanafunzi kuchagua masomo yanayoendana na vipaji na uwezo wao binafsi.
Mafunzo hayo yalifanyika kwa njia ya mtandao kuanzia Mei 13 hadi Julai 17, 2025, na yamehitimishwa rasmi leo, Septemba 23, 2025, katika hafla iliyofanyika katika makao makuu ya TET, Bamaga, jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa TET, Aneth Komba, alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Aneth amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza umahiri kwa wakuza mitaala ili kuwasaidia walimu kuandaa wanafunzi kuchagua masomo wanayoyapenda mapema, hususani wanapofikia darasa la sita.
“Tunaamini programu hii itawaongezea wakuza mitaala ujuzi na uwezo wa kufanya tafiti pamoja na kutumia mbinu bora za ufundishaji, hasa kwa walimu ambao ndio watakaoenda kuwafundisha wanafunzi shuleni.
“Walimu wakipata ushauri mzuri na wao wataenda kuwashauri vizuri wanafunzi, hii itawasaidia wanafunzi kufanya maamuzi sahihi kuhusu masomo wanayopaswa kusoma kulingana na vipaji na mapenzi yao,” amesema Aneth.
Ameongeza kuwa iwapo wanafunzi hawatapata mwongozo mzuri katika hatua za awali, kuna hatari ya kuchagua masomo wasiyoyaelewa au kuyapenda, jambo ambalo linaweza kuathiri mustakabali wao wa baadaye.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Aga Khan Education Services Tanzania, Dk Shelina Walli, ameipongeza TET kwa kushirikiana nao katika kuwajengea walimu uwezo wa kitaaluma, na kuwataka waendelee kupeleka walimu wengine zaidi kwa ajili ya mafunzo hayo.
“Tusipoishia hapa, bali tukiendelea kushirikiana, naamini tutajenga Taifa lenye watu wenye maarifa sahihi. Wanafunzi wanapaswa kujengewa uwezo mapema ili wawe na msingi mzuri katika maisha yao ya baadaye,” amesema Dk Shelina.
Aidha, amehimiza TET kushirikiana moja kwa moja na shule kwa kuwa walimu ndio wanaohusiana na wanafunzi katika kuwaelekeza na kuwashauri kuchagua masomo yanayowafaa.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wenzake, mmoja wa wakuza mitaala, Gwido Kalabona amesema: “Tutaenda kushirikiana na walimu walioko shuleni kwa karibu ili kuhakikisha elimu tuliyoipata inawafikia wanafunzi kupitia walimu wao. Tunatambua walimu ndio kiungo kikuu kati yetu na wanafunzi.