TUME YA MADINI YAWAALIKA WADAU KUTUMIA MAABARA YA KISASA

::::::::

Meneja wa Huduma za Maabara ya Tume ya Madini, Mhandisi Mwarabu Mvunilwa amewaalika wadau wa sekta ya madini nchini kutumia maabara ya kisasa ya Tume kwa huduma za uhakika na viwango vya kimataifa.

Akizungumza kupitia mahojiano maalum amesema kuwa maabara hiyo, ipo katika Jengo la TIRDO Complex, Msasani – Dar es Salaam, na imekuwa ikihudumia wachimbaji, wafanyabiashara wa madini, wawekezaji pamoja na taasisi mbalimbali kwa huduma za uchambuzi na ushauri wa kitaalamu.

Mhandisi Mvunilwa amesema kuwa maabara hiyo ya serikali imewekewa teknolojia ya kisasa ikiwemo mashine za X-Ray Fluorescence (XRF) na fire assay furnaces zinazotoa matokeo ya haraka, sahihi na yenye gharama nafuu.

 “Tunatoa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa vya ISO 17025. Matokeo yetu yanakubalika ndani na nje ya nchi, hivyo kuwa msingi wa uwazi katika biashara ya madini,” amesema.

Huduma zinazotolewa na maabara hiyo ni pamoja na uchambuzi wa madini ya metali kwa kutumia XRF, vipimo vya dhahabu na fedha kwa njia ya fire assay, acid digestion + AAS kwa metali za msingi, uhakiki kiasi cha dhahabu na utambuzi wa madini, pamoja na upimaji na maandalizi ya sampuli. Huduma nyingine ni vipimo vya unyevu na loss on ignition vinavyowezesha wachimbaji kupata taarifa sahihi za kijiolojia.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mvunilwa, maabara hiyo inaendeshwa na wataalamu waliobobea katika nyanja za jiokemia, madini na metallojia ambao hutoa matokeo yenye uhakika kwa ajili ya kusaidia maamuzi ya kiuchumi na kiuwekezaji. 

Ameongeza kuwa huduma hizo zimekuwa chachu ya kuongeza thamani ya madini na mapato ya serikali kupitia usahihi na uaminifu wa taarifa zinazotolewa.

Amesisitiza kuwa huduma za maabara hiyo si za ndani pekee bali pia zinatambulika kimataifa na hutumiwa na wateja kutoka mataifa mbalimbali, jambo linaloimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya madini duniani.

Wadau wa sekta ya madini wanahimizwa kutembelea maabara hiyo iliyopo TIRDO Complex, Msasani – Dar es Salaam au kuwasiliana kupitia barua pepe lab.coordinator@tumemadini.go.tz, simu 0733 010 338 au kupitia tovuti rasmi ya Tume ya Madini