Ukonga inavyozalisha mastaa wa kike Dar

KILE kituo cha Ukonga Basketball Academy ndicho kinachoongoza kwa ukuzaji wa vipaji vya wasichana katika Jiji la Dar es Salaam ambapo wengi wao wameonekana kutawala katika timu zinazoshiriki Ligi ya Kikapu mkoani humo (WBDL).

Baadhi ya mastaa wa kike wanaotesa katika ligi hiyo ni pamoja na Monalisa Kaijage, Witness Mapunda, Ana Marie na Noela Uwendameno waliosajiliwa na Jeshi Stars msimu huu.

Wengine ni Jesca Ngisaise, Judith Nyari, Hellen Simon, Shadya Amir, Kelta Kassim wanaokipiga JKT, Winfrida Chikawe, Amina Kaswa (Polisi), Hafsa Hasani na Hawa Athumani waliopo Vijana Queens.

Wachezaji wengine ni Tumaini Ndosi (Tausi Royals), Gloria Manda (DB Lioness) na Maria Kihivo (Pazi Queens).

Wachezaji hao wanaonekana kufanya vizuri katika WBDL huku Jesca akiongoza kufunga akiwa ametupia pointi 584.

Nyota huyo pia anashika nafasi ya kwanza kwa kufunga    eneo la mtupo mmoja wa ‘three points’ 59 huku Monalisa Kaijage akifunga 37. Mchezaji mwingine ni Noela Uwendameno aliyeongoza kutoa asisti akiwa nazo 32, huku Jesca akishika nafasi ya tano kwa asisti 23.

Akizungumzia mafanikio hayo, kocha wa kituo hicho, Denis Lipiki alisema walianzisha Ukonga Basketball Academy  mwishoni mwa 2014 baada ya kuona watoto wengi wakicheza kikapu katika maeneo ya Ukonga.

Lipiki alisema wengi wao walikuwa wametoka kuhitimu elimu ya msingi na kwamba, vipaji vingi vilishawishi kuanzishwa kwa kituo ambacho kimekuja kuwa tegemeo la timu nyingi.

“Bahati nzuri watoto wengi waliojitokeza walikuwa ni wa kike. Tuliweza kuwafundisha watoto hao mpaka wakaanza kuupenda sana mchezo wa mpira wa kikapu,” alisema.

“Siri kubwa ya ukuzaji wa wasichana wengi katika akademi yetu ni falsafa ya kumkuza mchezaji katika misingi ya muda mrefu.”

Aliwataja baadhi ya wachezaji waliobaki kituoni wakiandaliwa kuja kuwa mastaa tegemeo ni Janeth Maro, Happinnes Kombe,Thimina Haji, Bettim Kazinja, Mary Kajigili, Ester Kombe, Mariam Ramadhani na Judithi Nyangi, Dina Mussa, Zena Iddi na Najma Manji.