Vijana wabadili maganda ya matunda kuwa mkaa mbadala

Shinyanga. Ripoti ya mwaka 2024 inaonyesha kuwa matumizi ya mkaa mbadala nchini Tanzania yanaendelea kukua kwa kasi, ambapo takribani tani 45,000 ziliripotiwa kutumika ndani ya mwaka huo. Zaidi ya kaya 500,000 zimeanza kutumia nishati hiyo, jambo linaloashiria ongezeko la uelewa na kupokea kwa teknolojia mbadala ya nishati.

Hata hivyo, bado zaidi ya asilimia 85 ya Watanzania wanategemea kuni na mkaa wa miti kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia.

Mikoa inayoongoza kwa matumizi ya mkaa mbadala ni Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Dodoma, kutokana na urahisi wa upatikanaji wake na kampeni za uhamasishaji.

Mkoani Shinyanga, kikundi cha vijana kinachojulikana kwa jina la Tamba, kimebuni njia ya kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia maganda ya matunda.

Vijana hao wanakusanya taka za maganda ya ndizi, machungwa na miwa pamoja na miti ya mikungu ya ndizi, kisha kuzichakata na kubadilisha kuwa mkaa unaotumika nyumbani. Ubunifu huu umewasaidia kujipatia kipato na kuboresha maisha yao.

Leo Jumatatu Septemba 22, 2025 wakiwa katika Kata ya Majengo, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga vijana hao wamezungumza na Mwananchi wakieleza  namna wanavyofanikisha uzalishaji wa mkaa huo.

 Mwanzilishi wa kikundi hicho, Tamba Yahya amesema twalianza utengenezaji wa mkaa huo miaka mitatu iliyopita na utengenezaji wa mkaa huo huchukua siku mbili hadi tatu kutokana na kutumia vifaa duni.

“Tunatwangwa maganda kwa kutumia kinu na mara nyingi huwa tunatengeneza zaidi ya mawe 100 ya mkaa. Ndoo kubwa ya mkaa huu tunaiuza kwa Sh10,000,” amesema Yahya, huku akibainisha kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa mashine za kisasa za kuchakata taka hizo.

Mmoja wa wanakikundi, Elisante Aniel anasema taka za maganda ya ndizi, machungwa na miwa husagwa kwa kutumia kinu, kisha kuchanganywa na maji kabla ya kuundwa kuwa mawe ya mkaa.

“Changamoto kubwa ni vitendea kazi. Vifaa duni vinachelewesha uzalishaji na kutulazimisha kutumia nguvu nyingi katika hatua zote,” amesema Aniel.

Sophia Temba ni mmoja wa wateja wa mkaa huo, amesema umemsaidia kupunguza gharama za upishi kwa kuwa unachukua muda mrefu kumalizika.

“Kwa kawaida ninaweza kupikia kwa masaa matatu hadi manne kabla ya kuongeza mkaa mwingine. Kwa mkaa wa kawaida, ningehitaji kuongeza mara mbili au tatu zaidi,” amesema Sophia.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat), takribani watu bilioni 2.7 duniani hawana huduma sahihi za ukusanyaji taka, hali inayosababisha utupaji holela.

Kwa Tanzania, kati ya tani milioni 14 hadi 20 za taka huzalishwa kila mwaka, huku Jiji la Dar es Salaam likiongoza kwa kuchangia takribani asilimia 10 ya taka zote.

Duniani kote taka za mijini hufikia tani bilioni 2.1 hadi 2.3 kila mwaka, zikiwamo nguo, plastiki, vifungashio, vifaa vya kielektroniki na chakula.